Wanafunzi Tanzania kuwakilisha Afrika mashindano ya TEHAMA

13Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi Tanzania kuwakilisha Afrika mashindano ya TEHAMA

​​​​​​​WANAFUNZI wa Tanzania ni miongoni mwa washiriki wa fainali za mashindano ya kimataifa ya TEHAMA kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mashindano hayo yanayoandaliwa na Huawei, kaulimbiu yake ni "Connectivity, Glory, Future", ambapo kwa mwaka jana wanafunzi kutoka Tanzania na Nigeria walikuwa washindi wa jumla katika shindano hilo, hivyo kuwakilisha ukanda huo katika mashindano ya dunia.

Shindano hilo lilizinduliwa jijini Johannesburg, Afrika Septemba 10, mwaka huu  kwa njia ya mtandao. Shindano hilo linaaminika kuwa ndiyo kubwa zaidi barani Afrika kwa kushirikisha nchi 14 na kuhusisha wanafunzi zaidi ya 50,000.

Shindano la TEHAMA linaloandaliwa na Huawei, kwa mwaka huu limeshirikisha zaidi ya nchi 70 ulimwenguni, na kushindanisha wanafunzi 150,000 kutoka vyuo zaidi ya 2,000.

Tangu kuzinduliwa kwake miaka mitano iliyopita, shindano la TEHAMA la Huawei limeendelea kukua na kuwa shindano kubwa zaidi la TEHAMA barani Afrika.

Katika uzinduzi uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano, UNESCO na wanafunzi, Makamu Rais wa Huawei Afrika Kusini, Liao Yong, alielezea umuhimu wa mawasiliano katika zama hizi za kutokusogeleana.

“Utofauti katika mapokeo ya kidigitali unazidi kuongezeka katika kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na janga la Covid-19. Wakati watu wanapojisomea na kufanya kazi mtandaoni, wale wenye changamoto za kidigitali wanaathirika zaidi,” alisema Liao.

Katika semina ya mtandaoni iliyoandaliwa na UNESCO hivi karibuni, ilibainishwa kuwa miundombinu ya kidigitali ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu ya juu barani Afrika.

“Kufanya shindano hili la TEHAMA mtandaoni kwa kipindi hiki kuna thamani ya kipekee, inaonyesha kwamba Huawei kama waasisi wa miundombinu ya kidigitali Afrika pia tuko makini sana na mkakati wetu wa kuwekeza kwenye vipaji. Mkakati unajumuisha mambo matatu; kuwafundisha wataalamu wa TEHAMA kidigitali, kuhamasisha na kuwawezesha wanafunzi wa TEHAMA na kuongeza uelewa kwa watu wa kawaida.

Kampuni ya Huawei imewekeza zaidi katika kujiandaa na mashindano hayo kwa kufanya maonyesho kwenye vyuo 300, katika nchi 14 za Kusini mwa Jangwa la Sahara, na jumla ya wanafunzi 50,000 watashiriki. Mafunzo kuhusu mashindano haya yamesaidia zaidi ya wanafunzi 300 kupata ofa za kazi.

Aidha, mafunzo haya yamekuwa na umuhimu mkubwa kwa wanafunzi. mwanafunzi wa TEHAMA wa Tanzania, Emanuel Chaula, alifurahi  kwamba timu ya wanafunzi wa Tanzania ilikuwa moja ya timu kutoka nchi mbili zilizoshinda katika mashindano ya mwaka jana.

"Tulifanya kazi kwa bidii kama timu kwa sababu tulitaka kutumia fursa hiyo kusafiri kwenda China kushindana katika fainali za ulimwengu mzima. Tulitaka kuonyesha Afrika na ulimwengu kuwa Tanzania ni mdau mkubwa wa TEHAMA na tunataka kuwa sehemu ya ukuaji huo katika nchi yetu,” alisema.

Habari Kubwa