Wanafunzi vyuoni watakiwa kuwa wazalendo

06Dec 2019
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Wanafunzi vyuoni watakiwa kuwa wazalendo

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga,amewataka wanafunzi wa vyuo nchini, kuwa wazalendo na wasikubali kutumika na watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Mary Maganga, akiwatunuku vyeti wanafunzi wahitimu wa Chuo cha Uhasibu Arusha.

Maganga amesema hayo leo wakati wa mahafali ya 21 ya chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),,na kuwatunuku vyeti wahitimu 1323.

Amesema wapo watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania, pia wamekuwa wakiwatumia wanafunzi wa vyuo kama sehemu ya kufanikisha malengo yao.

“Wiki ijayao tunasherekea miaka 58, ya uhuru na miaka 57, ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kauli mbiu ni uzalendo,uwajibikaji na ubunifu ni msingi wa ujenzi wa uchumi wa Taifa,”amesema Maganga.

Maganga ametoa rai kwa wanafunzi wa vyuo waliohitimu mafunzo na wale waliobakia vyuoni kuzingatia kauli mbiu hiyo, ili kulinda amani na mshikamano wa nchi.

Licha ya kuzungumza hayo,amewataka wahitimu hao, kutumia elimu waliyoipata vyuoni  kuleta matokeo  chanya ya kiuchumi katika jamii kwa maslai ya taifa.

Pia amewataka wanafunzi wa vyuo nchini,kuwa na upendo,hekima,busara na waadilifu kwa watu waliowazunguka ili kuendelea kujenga misingi bora ya utamaduni wa kiafrika.

Mkuu wa Chuo hicho, Prof.Eliamani Sedoyeka, amesema chuo hicho,kinatarajia kuanzisha kozi saba mpya ya shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kukidhi matakwa ya watanzania.

Hata hivyo, amesema katika kuunga mkono jitihada za serikali kwa kutekeleza ilani ya chama tawala, chuo hicho kimejipanga kutoa elimu bora kwa kuweka mazingira rafiki ya wanafunzi kusomea.

Sedoyeka amesema wamefanikiwa kujenga zahanati ya chuo, bwalo la chakula, jengo kwa ajili ya idara ya uzamili litakalojumuisha madarasa na kumbi za mikutano na ujenzi wa mabweni.

Aidha amesema kwa kipindi cha mwaka 2019, chuo hicho kinaongezeko la wanafunzi 5,485 kutoka 3600.

“Sisi wahadhiri na walezi tunatarajia mtatumia maarifa,ujuzi na elimu mliyoipata hapa chuoni kuwatumikia watanzania wote kwa kuzingatia maelekezo ya Rais John Magufuli,’amesema Sedoyeka.

Habari Kubwa