Wanafunzi waishauri TAKUKURU taarifa za rushwa ngono vyuoni

30Jun 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanafunzi waishauri TAKUKURU taarifa za rushwa ngono vyuoni

WANAFUNZI wanaosoma vyuo mbalimbali mjini Shinyanga, wameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, kuwahakikishia usalama wa maisha yao, kwa kutunza siri za taarifa za rushwa ya ngono pale wanapokuwa wakizitoa kwenye taasisi hiyo.

Hayo yalibainishwa juzi na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali mjini Shinyanga, wakati wa utoaji elimu ya kutokomeza rushwa ya ngono vyuoni iliyokuwa ikitolewa na TAKUKURU.

Wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo ni kutoka Chuo cha Ualimu Shycom, Chuo cha Ufundi Stadi Veta, pamoja na Chuo cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi mkoani Shinyanga.

Baadhi ya wanafunzi hao akiwamo, Betina Mwashambwa kutoka Chuo cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi mkoani Shinyanga, alisema kuna wanafunzi wanaombwa rushwa ya ngono na wahadhiri wao, lakini wanaogopa kutoa taarifa hizo TAKUKURU, kwa kuhofia siri kuvuja na hatimaye kumharibia maisha yake.

“Tanaiomba TAKUKURU, mtuhakikishie usalama wa maisha yetu, kwa kutunza siri pale wanafunzi wanapokuwa wakitoa taarifa kwenu za rushwa ya ngono, kwa sababu unaweza kutoa taarifa kisha mhusika akaambiwa kuna mwanafunzi amekushtaki unamwomba rushwa, jambo ambalo litanifanya niishi maisha magumu chuoni,” alisema Mwashambwa.

Mwenyekiti wa Klabu ya kupinga rushwa wa chuo hicho, Kombeho Wiliam, aliwataka wanachuo kuacha kutunza siri za kuombwa rushwa ya ngono, bali watoe taarifa hizo TAKUKURU ili wasaidiwe na kupata haki zao, na siyo kuendelea kunyanyaswa kingono na kupewa maksi za bure.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Hussein Mussa, alisema wametoa elimu hiyo ya rushwa ya ngono kwa wanachuo, kwa sababu hatima ya ufaulu wao upo mikononi mwa wahadhiri, hivyo ni rahisi kwao kurubunika na kutoa rushwa hiyo.

Aidha, aliwatoa wasiwasi wanachuo hao kuwa taasisi hiyo itatunza siri kwa mwanafunzi yeyote ambaye atatoa taarifa za kuombwa rushwa ya ngono, huku akibainisha kuwa tangu wafungue dawati la rushwa ya ngono mwaka jana, wameshapokea taarifa mbili tu za wanachuo kuombwa rushwa hiyo.

Habari Kubwa