Wanafunzi wanusurika kifo kisa dereva kuchati na simu

12Jan 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanafunzi wanusurika kifo kisa dereva kuchati na simu

WANAFUNZI 30 wa shule ya msingi binafsi ya Little Treasure, iliyoko Manispaa ya Shinyanga, wamenusurika kifo baada ya kupata ajali wakati wakirejeshwa nyumbani kutokana na dereva wa basi hilo, Emmanuel Faustine (32), kuchati na simu ya mkononi huku akiendesha.

Wananchi wa manispaa ya Shinyanga wakiangalia basi la shule ya msingi binafsi ya Little Treasure, lenye namba za usajili T 183 AFE, baada ya kupata ajali na kujeruhi wanafunzi 30 katika eneo la Kalogo, barabara kuu ya kwenda jijini Mwanza juzi. PICHA: MARCO MADUHU

Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 9 alasiri katika eneo la Kalogo mjini hapa barabara ya Mwanza.

Basi hilo lenye namba za usajili T183 AFE likitokea shuleni na kusambaza wanafunzi nyumbani kwao na lilipofika eneo hilo, lilitumbukia mtaroni na kusababisha ajali.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Kamishina Msaidizi (ACP) Simon Haule, alisema wanafunzi 30 walikuwa wamesalia kwenye basi hilo na hakuna aliyepoteza maisha zaidi ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva ambaye alikuwa akichati na simu wakati akiendesha hatua ambayo ilisababisha kutumbukia mtaroni na kusababisha ajali huku akikimbilia kusikojulikana.

Kamanda Haule alisema kutokana na ajali hiyo, wanafunzi walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa matibabu.

“Jeshi la Polisi linamsaka dereva wa basi hili ambaye alikimbia mara baada ya kusababisha ajali, ili achukuliwe hatua kali za kisheria na liwe fundisho kwa madereva wengine ambao wamekuwa wakisababisha ajali za lazima na kugharimu maisha ya watu pamoja na kuwapatia ulemavu,” alisema Haule.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa, Dk. Albert Masigati alisema alipokea wanafunzi 30 na baada ya kuwapatia matibabu, 26 waliruhusiwa na kubakia wanne wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, ambaye aliwatembelea wanafunzi hao hospitalini hapo, aliwapongeza madaktari kwa kufanya kazi zao kwa ufanisi kuokoa maisha ya watoto hao.

Mboneko pia alitoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuwa makini wanapokuwa barabarani kwa kutii sheria ili kuepukana na ajali zisizo la lazima.

Habari Kubwa