Wanafunzi waonywa kuhusu siasa, ubaguzi

09Nov 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi waonywa kuhusu siasa, ubaguzi

WANAFUNZI wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/20 wamefundwa na kutakiwa kuzingatia kilichowapeleka chuoni na si kujiingiza kwenye siasa na ubaguzi.

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Kivukoni jijini Dar es Salaam, Prof. Shadrack Mwakalila, alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi wa astashahada, stashahada na shahada waliojiunga na chuo hicho.

“Zingatieni kilichowaleta hapa chuoni. Mmekuja kusoma ili mfanye vizuri katika mitihani yenu, hivyo mjiepushe na vitendo vinavyoashiria ubaguzi na masuala ya kisiasa,” alisema.

Prof. Mwakalila aliwataka wanafunzi hao wawe na nidhamu na kuwa na matumizi mazuri ya muda ili kufikia malengo waliyoyakusudia.

“Nimeamua kuzungumza nanyi kwanza kuwapongeza kwa kuchaguliwa katika chuo hiki cha Mwalimu Nyerer chenye historia iliyobeba jina la Mwasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.

Prof. Mwakalila aliwaeleza wanafunzi hao kuwa pindi wanapokutana na changamoto wasisite kuziwasilisha kwenye uongozi wa chuo ili zitatuliwe.

Aliwakumbusha wanafunzi hao kuwa chuo hicho kilipoanzishwa kilikuwa kwa ajili ya kuandaa viongozi wazalendo ili waende kuongoza nchi.

“Mpo kwenye chuo ambacho kitawajenga kimaadili na uzalendo kwa ajili ya kuwa viongozi wazuri pindi mtakapotoka hapa,” alisema.

Habari Kubwa