Wanafunzi wapata ajali wakirejea shuleni

30May 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanafunzi wapata ajali wakirejea shuleni

WANAFUNZI kutoka vyuo mbalimbali na wanafunzi wa kidato cha sita wanaosoma jijini Mbeya, wamenusurika kifo baada ya basi ya Premier lenye namba za usajili T, 629 AET, walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Mbeya, jana saa 3 asubuhi, kupata ajali katika eneo la Ngaganulwa Usanda, wilayani ...

Shinyanga.

Abiria walionusurika kwenye ajali hiyo akiwamo Justice Alyoce, mwanafunzi wa kidato cha sita, alisema wakati wakiwa njiani wakitokea Mwanza, basi hilo lilikuwa likifukuzana na Abood na walipofika eneo hilo wakapata ajali.

Alisema katika eneo hilo la Ngaganulwa, basi la Abood lililokuwa mbele lilisimama upande wa kushoto na upande wa kulia kulikuwa na basi jingine la Allys, ndipo dereva la basi la Premier alipoanza kufunga breki na kumshinda na kisha kuanguka.

“Wakati tukitokea Mwanza kwenda Mbeya shuleni na wengine vyuoni, tulipokuwa njiani basi letu la Premier pamoja na Abood yalikuwa yakifukuzana huku madereva wakipigiana honi walipokuwa akimpita mwezake, na tulipofika hapa wakati tukiwa mwendokasi ndipo tukakutana na mabasi yamesimama na hatimaye kupata ajali,”alisema Aloyce.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi, dereva wa basi la Premier alipofika eneo hilo na kukuta mabasi mawili yamesimama pande zote basi lilimshinda na hatimaye kuanguka.

Alisema basi hilo lilikuwa limebeba abiria 59, wengi wao wakiwa wanafunzi wa kidato cha sita pamoja na vyuo, huku akiwataja majeruhi saba wa ajali hiyo kuwa ni Thabiti Abdul, Swaum Kisandu, Mohamed Nyerere, Betha Minami, Mohamed Ahmed, Ilham Yahya, pamoja na Haida Hassani.

Alisema Majeruhi hao wote wamepata majeraha katika maeneo mbalimbali ya viungo vya miili yao na kukimbizwa kituo cha afya Tinde, kilichopo karibu na eneo la ajali, huku kukiwa hakuna kifo na kubainisha wanamtafuta dereva wa basi hilo ambaye amekimbia.

Habari Kubwa