Wanafunzi wapya Muleba wafundwa

18Jan 2022
Lilian Lugakingira
Muleba
Nipashe
Wanafunzi wapya Muleba wafundwa

WANAFUNZI waliojiunga na kidato cha kwanza katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wametakiwa kutunza miundombinu ya madarasa na kuzingatia watakayofundishwa na walimu ili wafaulu vizuri na kutimiza ndoto zao za kimaisha.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila, wakati wa ziara katika shule za sekondari za Kaigara, Anna Tibaijuka, Kasharunga na shule mpya ya sekondari ya Kasharunga (Kiteme) kwa ajili ya kukagua mwitikio wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti shuleni.

Akizungumza na wanafunzi hao Kayandabila, amesema kuwa wamepata nafasi ya kusomea katika mazingira yaliyobora hivyo, anatarajia watafanya vizuri katika masomo maana malipo pekee wanayoweza kumlipa Rais Samia Suluhu Hassan ni kufaulu.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutoa taarifa za watoto wa kike waliochaguliwa kujiunga na kidato cha ambao wameolewa kwa shinikizo la wazazi au kwa maamuzi ya watoto wenyewe, ili serikali ichukue hatua dhidi yao na kuwarudisha shuleni.

"Lengo la serikali ni kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanakwenda shule bila kujali kama ni wa kiume au wa kike, tutawafuatilia wote na kuhakikisha wanaendelea na elimu," amesema mkurugenzi huyo.

Naye, kaimu afisa elimu sekondari wa Wilaya ya Muleba, Masatu Chisumo, amewataka walimu kuanza ratiba za vipindi mara moja ili kuwezesha wanafunzi kuelewa haraka kutokana na kuwa na muda wa kutosha kujifunza.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari ya Anna Tibaijuka, mwalimu Paulo Mligo, ametoa shukrani kwa Rais kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya ya kisasa ambavyo vimesaidia kupunguza uhaba na kuahidi kwamba watavitunza vyumba hivyo ili viweze kuwasaidia wanafunzi wengine kwa miaka ijayo.

Mmoja wa wazazi ambao watoto wao wamejiunga na kidato cha kwanza wilayani humo, Gosbert Gervas, ameishukuru serikali kuwajengea vyumba vya madarasa watoto wao kwa kutumia fedha za Uviko 19, na kwamba hatua hiyo imesaidia kuwapunguzia wazazi adha ya michango ya vyumba vya madarasa.

"Kuna baadhi ya watoto hasa wa kijiji cha Kiteme walikuwa wakitembea umbali mrefu kutoka kijijini hapo kwenda shule ya sekondari Kasharunga, hali hii ilipelekea wazazi kuwapangia vyumba vya kuishi karibu na shule, matokeo yake baadhi ya watoto walibeba mimba na hata kuharibikiwa kwa kukosa uangalizi wa karibu wa wazazi," amesema.

Amesema kuwa sasa wamejengewa shule mpya ya Kasharunga (Kiteme) ambayo itawapunguzia watoto kutembea umbali mrefu na hata kuwafanya kumaliza masomo yao salama kutokana na uangalizi wa karibu wa wazazi.

Wilaya ya Muleba ilipokea zaidi ya Bil 4.1 ambazo zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 208 katika shule za sekondari.

Habari Kubwa