Wanafunzi wasimamishwa masomo, wapigwa viboko

03Mar 2016
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Wanafunzi wasimamishwa masomo, wapigwa viboko

WANAFUNZI 10 wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Namabengo, Namtumbo mkoani Ruvuma, wamesimamishwa shule kwa wiki tatu kwa utovu wa nidhamu na kushawishi wenzao kufanya maandamano bila kibali.

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako.

Wanafunzi hao ambao walikuwa kati ya 106, waliandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kumpelekea malalamiko dhidi ya Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Shaibu Champunga, kwa madai kuwa ana lugha chafu na vitisho.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Alkwin Ndimbo, alisema baada ya wanafunzi kuandamana, zilifanyika jitihada za kuwarudisha shuleni ili kubaini tatizo lililojitokeza.

Alisema katika kufanya hivyo, alimwagiza Ofisa Elimu ya Sekondari wa Wilaya, Patrick Athanas kuchukua hatua za haraka kwa kukutana na viongozi wa shule na wanafunzi.

Ndimbo aliesema baada ya Athanas na uongozi wa shule kukutana na wanafunzi wote, ilibainika kuwa wanafunzi hao walifanya maandamano kutoka Namabengo hadi Mlete, umbali wa kilomita 16 bila kufuata utaratibu.

Alisema kitendo hicho ni cha utovu wa nidhamu kwa kuwa walivunja kanuni na sheria za shule kwa kuondaka eneo la shule bila idhini ya walimu na walikiri kufanya hivyo.

Kutokana na kosa hilo, uongozi wa shule uliamuru wanafunzi 96 wachapwe viboko vitatu kila mmoja huku wengine 10 waliokuwa vinara wa maandamano hayo, wakisimamishwa masomo.

Mbali na kusimamishwa, wanafunzi hao wametakiwa kwenda na wazazi wakati wa kurudi na kwamba watapewa adhabu zaidi.

Kuhusu tuhuma dhidi ya mwalimu huyo, alisema si za kweli kwa kuwa hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyethibitisha walipokuwa wakihojiwa.

Mwalimu huyo alikuwa akituhumiwa kutoa lugha za vitisho na matusi kwa wanafunzi, kuwachapa viboko visivyo na idadi, kuingia kwenye bweni la wanafunzi wa kike nyakati za usiku bila kuongozana na matroni na kuwalazimisha kufanya mapenzi pamoja na kuwazuia wanafunzi wa kike kulala bwenini.

Habari Kubwa