Wanafunzi watano wagongwa, wafariki dunia wakitoka shuleni

14Feb 2020
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Wanafunzi watano wagongwa, wafariki dunia wakitoka shuleni

WANAFUNZI watano wa Shule ya Msingi Ndelenyuma iliyoko katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, wamefariki dunia na mwingine kujeruhiwa kutokana na kugongwa na gari wakati wakitoka shuleni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, picha mtandao

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alidai tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nane mchana kwenye barabara ya kutoka Njombe kwenda Songea, ambayo wanafunzi hao walikuwa wanatembea kandoni mwake.

Alidai wanafunzi hao waligongwa na gari lenye namba za usajili T 443 AQT aina ya Landcruser, mali ya Kampuni ya Camsat.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Glory Kilasi (12), Ushindi Juma (12), Isaya Mkani (13), wote wa wanafunzi wa darasa la nne, Evaristo Miligo (10), mwanafunzi wa darasa la Pili, na Victor Luoga, (10), mwanafunzi wa darasa la kwanza.

Kamanda Maigwa alimtaja aliyejeruhi kuwa ni Hilda Kilasa (12), mwanafunzi wa darasa wa la nne, ambaye baada ya ajali hiyo, alikimbizwa katika hospitali ya mkoa kwa ajili ya matibabu na anaendelea vizuri.

Alidai kuwa gari hilo lililokuwa linatoka Njombe kwenda Songea katika Kijiji cha Ndelenyuma, liliacha njia na kuwagonga wanafunzi hao sita kisha likapinduka.

Alidai gari hilo lilikuwa linaendeshwa na mwanamume aliyemtaja kwa jina moja la Salum na baada ya ajali hiyo, alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Kamanda Maigwa alidai chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye hakujali hali ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika kijiji hicho.

Alidai kuwa baada ya kugongwa, wanafunzi hao walidondokea mtaroni na kwamba, watatu walisombwa na maji na miili yao kuopolewa takribani mita 100 kutoka eneo la tukio na jitihada zinafanywa kumkamata dereva huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema, alisema taratibu za mazishi zilikuwa zinaandaliwa na miili ya wanafunzi hao ilitarajiwa kuzikwa katika kijiji hicho jana mchana, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, akitarajiwa kuongoza maziko hayo.

Habari Kubwa