Wanafunzi wenye mahitaji watakiwa kujituma kusoma

23Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Chalinze
Nipashe
Wanafunzi wenye mahitaji watakiwa kujituma kusoma

WANAFUNZI wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi ya Chalinze mkoani Pwani wamehimizwa kusoma kwa juhudi ili kutengeneza maisha yao ya baadaye, huku wakipewa changamoto ya kujitahidi kila wakati kuwa bora katika masomo na kwa kila kitu wanachofanya.

Hamasa hiyo imetolewa na Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Samora jijini Dar es Salaam, Zubeider Haroun, wakati akikabidhi mifuko 75 ya saruji kwa shule hiyo ikiwa ni hatua ya benki kuboresha miundombinu shuleni hapo hususani kwa kujenga choo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Zubeider aliwasihi wanafunzi hao kuwa elimu inaweza kuwapeleka mbali na kutimiza ndoto zao, kwa hivyo wanahitaji kusoma kwa juhudi katika masomo yao huku akiwasisitiza kutokata tamaa hasa wanapopata changamoto katika safari zao za masomo.

“Kwa hivyo nawasihi muweke juhudi katika masomo yenu kwa ajili ya faida ya maisha yenu ya baadae kwa kuwa elimu ni ufunguo, ambao unafungua milango ya maisha yote. ” alisisitiza

Aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kusaidia maendeleo ya elimu ikiwamo kwa wale walio na mahitaji maalum ili kuboresha mfumo wa elimu jumuishi nchini.

“Tumejitolea kusaidia ujenzi wa hitaji hili muhimu la miundombinu ya katika shule hii ili kuboresha upatikanaji wa elimu hususani kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum,’’ alisema.

Pia, Zubeider alitoa wito kwa taasisi zingine na watu binafsi kuchangia kwa shule na vituo vya elimu kama nguzo muhimu kuelekea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akipokea msaada huo Aufemia Ngweta, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, aliishukuru Benki ya NBC kwa msaada huo na utashi wake katika kusaidia ukuaji wa elimu katika wilaya hiyo. Pia alitoa wito kwa wadau zaidi kusaidia shule hiyo.

"Hapa shuleni kuna watoto wenye ulemavu tofauti, kuna wale walio na ugonjwa wa kupooza kwa ubongo ambao wanahitaji vifaa vingi vya kuchangamsha akili zao ili waweze kujifunza vitu mbalimbali kama ufundi na ujuzi mwingine kwa maendeleo yao ya baadaye. Kwa hivyo juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha tunawafundisha vyema,” alisema Ngweta.

Alimshukuru pia Bi Zubeida kwa kuwahamasisha wanafunzi hao, akibainisha kuwa ni matumaini yake wanafunzi hao watabadilisha mawazo yao na kuthamini.

Wanafunzi walishukuru Benki hiyo kwa msaada huo, huku wakiaahidi kufanya vizuri kitaaluma sambamba na kutoa wito kwa jamii iendelee kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao.

Habari Kubwa