Wanafunzi wote waliofaulu la 7 kuingia sekondari

04Jan 2022
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanafunzi wote waliofaulu la 7 kuingia sekondari

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema wanafunzi 9,780 waliofaulu darasa la saba mwaka jana, wataingia kidato cha kwanza Januari 17, mwaka huu, baada ya vyumba vya madarasa 15,000 kukamilika ujenzi.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA), alisema nguvu kubwa ya serikali ni kuboresha elimu ili wanafunzi wasome vizuri, na wajibu wa watendaji ni kusimamia na kuchapa kazi ili malengo yaliyowekwa yafikiwe kwa ufanisi.

Alisema madarasa hayo yamejengwa kwa fedha za UVIKO-19 na sasa nchi ina uhakika wanafunzi wote waliofaulu wataendelea na masomo yao na hakuna atakayekaa nyumbani.

Alisema ndani ya miezi tisa wizara hiyo imepata fedha za kuendeleza elimu ya juu, Dola za Kimarekani milioni 425 sawa na Sh. milioni 982, na kwamba mradi mwingine ni kuimarisha elimu ya sekondari utakaogharimu Dola za Marekani milioni 500 sawa na Sh. trilioni 1.15 ambazo zimepelekwa kwenye halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari 245.

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, katika kila eneo zimetengwa Sh. milioni 600 kwa ajili ya kujenga shule mpya na kwamba hadi mwaka 2025 zitajengwa shule za sekondari za wasichana 26 na kwa kuanzia wameanza ujenzi kwenye mikoa 10 na fedha zimeshapelekwa.

 “Nitakuwa mkali kweli kweli, sitakubali mtu achezee hata senti tano ya fedha ambazo zimeletwa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu, naiomba Bodi isimamie kikamilifu, waulize sana wakati mwingine watendaji wanaona kama bodi inapitiliza, lakini watambue ndiyo yenye dhamana itapitiliza vipi, naomba simamieni vizuri mtu asiwatie woga kwa namna yoyote ile,” alisema.

MAKTABA MTANDAONI

Prof. Ndalichako alisema ni muhimu bodi hiyo ikakamilisha uanzishaji wa maktaba mtandaoni ili kuwezesha Watanzania wengi kujisomea vitabu na machapisho kulingana na mahitaji ya rika zote.

Alisema bajeti imeongezeka Sh. milioni 424.2 hadi Sh. bil. 1.4 zilizowezesha kumudu gharama za uwekezaji kuanzia ofisi za tarafa hadi taifa, huku ikiongezeka kutoka Sh. milioni 500 mwaka 2020/21 hadi Sh. bilioni 10.5 mwaka 2021/22, na kwamba lazima zisimamiwe kufikia malengo husika.

“Shilingi bilioni mbili zitatengeneza maktaba mtandao, bilioni tatu, ukarabati wa jengo la Maktaba Kuu ya Taifa, shilingi bilioni 3.5 za ujenzi wa maktaba Wilaya ya Chato na shilingi bilioni 1.5 ni za ununuzi wa samani katika vituo 43 vya maktaba na shilingi milioni 500 kwa ajili ya jengo la maktaba ya Arusha,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, ni muhimu kuwa na vitabu vya kuwawezesha wananchi kujenga uwezo kwenye shughuli zao za kila siku, kwa kuhakikisha wanataaluma, wakulima au wajasiriamali wanapata vitabu na machapisho ya kuboresha shughuli zao kwa kuwa lengo la nchi ni kuendeleza utamaduni wa kujisomea kwa kutumia maktaba zitakazojibu kiu yao.

Aidha, alisema majukumu ya bodi ya maktaba yameainishwa kwenye Sheria ya Bodi Namba 6 ya Mwaka 1975, na kwamba ni muhimu kumshauri kama inakidhi matarajio au kuna haja ya kuifanyia marekebisho ili iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini na duniani, huku akitolea mfano maktaba mtandao, sheria haijalizungumzia na kwamba ni muhimu kuangalia utoshelevu wake.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Rwekaza Mukandara, alisema watatekeleza majukumu yao kwa umakini na uadilifu katika kuboresha huduma za maktaba nchini, ambacho ni kisima cha ujuzi na maarifa, kwa kuwa kuna mkusanyiko wa maandiko ya masomo ya fani mbalimbali, ambayo yamemwongezea binadamu uelewa wa mazingira anamoishi na mbinu za kukabiliana na changamoto.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa BOHUMATA, Dk. Mtoni Ruzegea, alisema baadhi ya vipaumbele ni kwamba kila mwandishi au mchapishaji wa ndani ya nchi atawajibika kupeleka nakala mbili ya kazi zake kwa ajili ya kuhifadhiwa, kuwajengea uwezo na kuwaendeleza watumishi kimasomo.

Habari Kubwa