Wanahabari wakumbushwa weledi habari za magonjwa ya mlipuko

12Sep 2020
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Wanahabari wakumbushwa weledi habari za magonjwa ya mlipuko

Waandishi wa habari mkoani Kagera wametakiwa kupata habari kutoka kwa vyanzo sahihi na  mamlaka zinazohusika zikiwamo zinazohusu magonjwa ya mlipuko ikiwamo corona, ili kuepuka kutoa taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kusababisha taharuki kwa jamii na kuzua hofu.

Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa Hospitali ya Rufaa Bukoba, Dk. Mussa Sweya wakati akitoa mada kuhusu magonjwa ya mlipuko kwa waandishi wa habari zaidi ya 40 ambao ni wanachama wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Kagera -KPC- kutoka katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Dk. Sweya amesema kuwa watu  wanaweza kupoteza maisha pindi yanapotokea magonjwa ya mlipuko kama corona na ebola  kutokana na hofu, na kuwataka wananchi kuzingatia maelekezo kutoka katika mamlaka zinazohusika ili kuepuka kukumbwa na hofu.

"Yanapotokea magonjwa ya mlipuko vyombo vya habari hutegemewa kuutaarifu umma hatua wanazopaswa kuzichukua kujikinga, lakini taarifa hizi lazima zitolewe na vyombo vyenye mamlaka, na sio kila mtu ana uwezo wa kuyazungumzia ili kuepusha upotoshaji kwa wananchi" amesema.

Mwandishi wa habari mkongwe Joas Kaijage amewataka waandishi wa habari kujiandaa kikamilifu wanapokwenda kuandika habari katika maeneo yenye migogoro, vurugu na maandanano, ili wasiweze kudhurika.

Kaijage amesema kuwa kabla ya mwandishi kwenda eneo la tukio inapaswa kufanya mahesabu na kupata majibu ya maswali hayo na kuwa endapo majibu yataonyesha madhara kwake ni makubwa kuliko usalama wake basi asiende kufanya kazi hiyo.

"Lakini mwandishi anaweza kujipanga upya na kufanya mahesabu mapya ambayo yataweza kupunguza madhara kwake na endapo atabaini madhara yamepungua basi anaweza kuendelea kufanya kazi hiyo" amesema.

Amesema, mwandishi anapokwenda eneo la tukio anapaswa kurudi na vitu viwili muhimu ambavyo ni habari lakini pia uhai wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa KPC, Mbeki Mbeki amewataka waandishi wa habari kutii sheria zilizopo ili kuepuka kuadhibiwa.

"Hakuna yeyote aliyeko juu ya sheria, lazima kila mwandishi afanye kazi zake kwa mujibu wa sheria ikiwamo ya Huduma ya Habari na Makosa ya Kimtandao na nyinginezo zinazowagusa katika taaluma hii, ndipo mtakuwa salama"amesema Mbeki.

Kwa mujibu wa Katibu wa KPC, Livinus Feruzi, mafunzo kuhusu magonjwa ya mlipuko ikiwamo COVID-19 yamefadhiliwa na shirika la SIDA kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania - UTPC. 

Habari Kubwa