Wanahabari wafundwa matumizi ya utafiti

23Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanahabari wafundwa matumizi ya utafiti

WAANDISHI wa habari wametakiwa kutumia  matokeo  ya  utafiti wa kitaalamu kutoa taarifa zitakazosaidia kuleta mabadiliko katika jamii.

Mkurugenzi  wa Utafiti wa Kimkakati wa Taasisi ya Utafiti wa 
Kuondoa Umaskini (Repoa), Dk. Jamal Msami, alisema hayo jana kwenye mjadala wa ukuaji wa uchumi wa ndani uliondaliwa na taasisi hiyo.

Alisema ili kupata  maendeleo ya uchumi wa ndani ni muhimu kutumia utafiti uliopo ili kuchochea mabadiliko  ya kiuchumi kwa kuwianisha utafiti huo na hali halisi za wananchi lengo hasa likiwa ni kuibua fursa zilizopo.

 “Limekuwa suala la kawaida tunapozungumza au mwanataaluma anaposema uchumi umekua kunatokea miguno na watu kushindwa kuelewa  kuwa uchumi unakua kwa maana kipato chake mfukoni au wananchi wote kwa ujumla,” Dk. Jamal alisema.

Dk. Jamal pia alisema ni muhimu pawapo mfumo rasmi wa kuwasaidia  wananchi wa kawaida  kwa kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali katika shughuli za uzalishaji mali hali inayosababisha kutokupata  thamani halisi ya uzalishaji wao na kutotambua fursa zitakazowasaidia kiuchumi.

“Unakuta  mkulima analima, halafu anahangaika anatafuta soko bila kujua atakutana na nani sokoni ndiyo maana wengine wanaamua kuwatumia madalali ingawa pia huo si mfumo rasmi,” alisema.

Naye  Mhariri Mtendaji  Mkuu  wa Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu, alisema utafiti ni muhimu kwa kuwa unasaidia kulijua tatizo, hivyo kutafuta majawabu sahihi na hatimaye kuhakikisha Watanzania hasa wa hali ya chini wanapata fursa za kiuchumi  katika nchi yao.

“No research no right to speak (hakuna haki ya kuzungumza bila utafiti). Utafiti unatusaidia kujua tatizo na kupata majawabu sahihi kulingana na tatizo husika,” alisema Machumu.

Mkurugenzi wa Utafiti wa Repoa, Dk. Blandina Kilama, alisema wananchi  wa kawaida wana uelewa  tofauti kuhusiana na umaskini,  hivyo ni muhimu kuangalia viashiria na vigezo  mbalimbali katika kutathmini hali ya uchumi nchini.

”Tulipomuuliza  baba mmoja  kuhusu uelewa wake kuhusu umaskini, alisema kwetu sisi mtu yeyote anayeshindwa  kumpeleka mtoto wake shule binafsi  ni maskini. Hapo ni Kilimanjaro. Huko Kakonko mtu mmoja alisema mimi si maskini kwa sababu nina uwezo wa kula milo miwili kwa siku kwa hiyo sisi kama wachambuzi tunaongeza na zile standards (viwango)  nyingine tunazozijua ,” alisema.

Habari Kubwa