Wanahabari waombwa kushiriki kampeni uchangiaji damu

08Jun 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Wanahabari waombwa kushiriki kampeni uchangiaji damu

WANAHABARI wameombwa kushirikiana na mpango wa Taifa wa damu salama katika kuandaa kampeni za uchangiaji damu kwa vijana ili kusaidia upatikanaji wa damu nchini kwa lengo la kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji.

Akizungumza wakati wa utoaji elimu kwa wanahabari kuhusu kampeni ya  uchangiaji damu, iliofanyika kwa njia ya mtandao Meneja wa  Kanda kitengo cha damu salama Nyanda za Juu Kusini Dk. Lelo Baliyima amesema, kwa kuwa muhimili wa habari una nguvu katika jamii basi wautumie katika kuhamasisha  vijana wachangie damu.

Dk. Lelo amelisema sababu ya kuhamasisha vijana kuchangia damu ni kutokana na takwimu zinaonesha damu ya vijana ni salama kwa kiwango kikubwa  ambapo asilimia 9 chini ya miaka 35 na asilimia 22 zaidi ya miaka 35.

Amesema, vijana wanajitoa sana katika kusaidia jamii ambapo asilimia 80 ya wachangia damu kwa sasa ni wale walio chini ya miaka 35, pia wanapenda kujaribu vitu ikiwemo kuchangia damu.

Aidha, amesema vijana wanapatikana kwa urahisi pale wanapohitajika na ni rahisi kwa kundi hilo kuhamasishana kuchangia damu kuliko kwa watu wazima.

Hata hivyo amesema, changamoto iliopo kwa vijana kutochangia damu ni kutokana na vituo vya kuchangia damu kutokuwa karibu na mahala wanapoishi au kutokuwa na taarifa za maeneo ya jirani wanapowexza kuchangia damu  na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu uchangiaji damu.

“kutokana na changamoto hizo wanahabari tushirikiane  katika kutafuta njia bora za kuwafikia vijana na kuwapa elimu ya uchangiaji damu,tusaidiane kuvitangaza vituo vya damu salama ili vijana waweze kutambua vilipo na kufika kwa urahisi,tutumie vyombo vyetu kuwapa elimu ya kupambana na  uuzwaji wa damu ambao umekuwa ukifanyika kwenye baadhi ya hospitali kwani damu haiuzwi inatolewa bure,”amesema Dk. Lelo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya ukusanyaji damu Dk. Avelina Mgasa amesema,siku ya wachangiaji damu ufanyika Juni 14,kila mwaka duniani kote  ambapo kwa mwaka huu kitaifa nchini hapa yatafanyika jijini Dodoma   na maadhimisho kikanda yatakuwepo katika Kanda zote za damu salama.

Habari Kubwa