Wanahabari wapewa somo kuhusu SADC

18Jul 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Wanahabari wapewa somo kuhusu SADC

MKURUGENZI wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abas, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuonesha changamoto zinazoikabili Serikali au zinazoweza kuikwanza katika kutimiza ajenda zake kwa faida ya wananchi.

MKURUGENZI wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abas.

Alisema vyombo hivyo vinawajibika kueleza ukweli, kutumia utafiti na kutumia lugha ya kiungwana pale penye mapungufu.

Dk. Abas alisema hayo mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo maalum kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa waandishi wa habari, yaliyofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ).

Mafunzo hayo maalumu ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya SADC yalifanyika mjini Morogoro kwa awamu mbili na kushirikisha jumla ya waandishi wa habari 60 wa kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.

Dk. Abas alisema mafunzo hayo yamelenga kuwapa elimu na uelewa mpana waandishi wa habari ambao ni wawakilishi na mabalozi wa jamii ya Watanzana zaidi ya milioni 55, wanaosubiri kwa hamu kujua mengi kuhusu SADC wakati Tanzania ikielekea kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali 16 za SADC utakaofanyika nchini mwezi ujao.

Alitaja wajibu mwingine kwa vyombo vya habari ni kwenda mbali kabisa na kauli za kila siku za viongozi, wanasiasa na wanaharakati kwa kuwapa jukwaa wananchi wa kawaida na wadau wengine kupaza sauti zao.

“Huu wakati pia tuwape wananchi fursa ya kueleza matarajio yao kuhusu SADC, wangependa kama Taifa tufaidike nini kwenye SADC na watoe maoni yao mbalimbali kuhusu mkutano ujao,” alisema Dk. Abas .

Dk. Abbas alisema ni matarajio yake kuna vyombo vya habari vinatenga muda wa kutosha kufuatilia masuala ya historia ya Tanzania na SADC kwa kuwa wapo viongozi wengi wa Jumuiya hiyo waliowahi kuishi nchini .

Mwaka huu Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya hiyo umepangwa kufanyika jijiji Dar es Salaam Agosti 17 na 18, mwaka huu na Rais John Magufuli atapokea kijiti kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mkutano huo utakwenda sambamba na maonesho ya wiki ya viwanda kwa nchi wanachama ambayo yatafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere , Dar es Salaam kuanzia Agosti 5 hadi 9, mwaka huu, na kaulimbiu ni “Mazingira Wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda”.

Mwakilishi wa GIZ, Dagmore Tawonezvi kutoka Botswana, ambaye pia ni Meneja wa programu ya kuimarisha utengamano baina ya nchi za SADC, alisema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuwahabarisha wananchi kuhusu Jumuiya hiyo.

Habari Kubwa