Wanahabari watakiwa kupinga matukio ya ukatili

25Nov 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanahabari watakiwa kupinga matukio ya ukatili

WAANDISHI wa habari hapa nchini, wametakiwa kutumia kalamu zao kuelimisha jamii, kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Hayo yamebainishwa leo na Mkufunzi Mwandamizi wa waandishi wa habari, Alakok Mayombo, kutoka Internews wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari, juu ya kuandika habari za kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia, katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili huo.

Amesema waandishi wa habari kwa kutumia kalamu zao wanauwezo mkubwa wa kuibadilisha jamii kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

"Waandishi wa habari mnauwezo mkubwa sana kuibadilisha jamii kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia kupitia kalamu zenu na hata kuondoa masuala ya mila na desturi kandamizi," amesema Mayombo.

Naye Musa Juma, ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo, amewasisitiza waandishi wa habari, katika kuandika habari za matukio ya ukatili wa kijinsia wazingatie usawa katika habari zao.

Kwa upande wake Ali Sultani, akitoa mafunzo hayo, amewakumbusha wanapokuwa wakitaka kuandika habari lazima wawe na wazo na kujua nini wanacholenga katika habari hiyo, pamoja na kufuata kanuni na maadili ya uandishi.

Nao baadhi ya waandishi wa habari ambao wameshiriki mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Internews, kwa nyakati tofauti wamesema watayatumie katika kuhabarisha umma juu ya kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Habari Kubwa