Wanahisa NICOL wapitisha gawio la bilioni moja

05Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Wanahisa NICOL wapitisha gawio la bilioni moja

WANAHISA wa Kampuni ya NICOL Investment PLC, wameidhinisha gawio la Sh, 1,047, 792, 178 kwa mwaka wa fedha unaoishia 2021 ambapo kwa kila hisa moja itatolewa Shilingi 17.

Mwenyekiti wa Kampuni ya NICOL Investment PLC Dk. Gideon Kaunda akiongoza Mkutano Mkuuwa mwaka wa wanahisa uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wanahisa hao walipitisha mapendekezo ya menejimenti ya kutoa gawio la Sh bilioni 1.045.

Hayo yalifikiwa mwishoni mwa wiki wakati wa Mkutano Mkuu wa saba wa mwaka kwa wanahisa wa kampuni hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Malipo hayo kwa wanahisa kwa mujibu wa mkutano huo yanatarajiwa kulipwa kabla ya tarehe 30 Desemba mwaka huu kwa wanahisa wote walioko kwenye kitabu cha orodha ya wanahisa.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Erasto Ngamilaga, alisema kampuni hiyo ilikuwa katika matatizo siku za nyuma lakini sasa imeanza kupata mafanikio makubwa na wanahisa wanafurahia manufaa wanayopata.

Baadhi ya wakurugenzi wa Kampuni ya NICOL Investment wakisoma nyaraka wakati wa mkutano huo ambao ulifanyika mwishoni mwa wiki ambapo wanahisa hao walipitisha mapendekezo ya menejimenti ya kutoa gawio la Sh bilioni 1.045.

Alisema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na menejimenti mpya, kampuni hiyo imetangaza kutoa gawio kwa wanahisa wake ambalo litalipwa mwaka huu.

“Tumekuwa na mkutano mzuri ambapo wanahisa wengi wameonyesha kufurahishwa na mwenendo wa kampuni kwa kupata faida kutokana na uwekezaji ilioufanya kwenye maeneo mbalimbali,” alisema

Alisema kampuni inaenda kutekeleza malengo makubwa ya kiuwekezaji kwa kuwekeza kwenye maeneo mengine mengi yenye kuleta faida na kutawanya uwekezaji ili kupata faida .

 Baadhi ya wanahisa wa Kampuni ya NICOL Investment wakisikiliza mwenendo wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanahsia wa kampuni hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Alisema kampuni hiyo awali ilikuwa kwenye mlolongo mkubwa wa matatizo kwa uongozi wa zamani lakini uongozi mpya umejitahidi kwa kiwango kikubwa kuyatatua na hivi sasa wanahisa wanafurahia matunda.

“Tunaona fahari kwamba wanahisa sasa wanafurahi kwasababu wanapata kile walichokuwa wakistahili na ni matarajio yetu kuwa huko mbele kutakuwa na nuru kubwa sana kwa kampuni kuwa na faida,” alisema

Alisema mwaka 2020 walipendekeza gawio la Sh 10 kwa kila hisa ambalo kila mwanahisa amelipwa na sasa  kutokana na matokeo mazuri ya kifedha kwa kipindi cha nusu mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2021, ambapo faida baada ya kodi iliongezeka hadi Sh bilioni 3.8 kutoka Sh bilioni 2.2 mwaka uliopita kipindi kinachofanana.

Alisema faida baada ya kodi kufikia mwisho wa 31 Desemba 2021 inakadiriwa kufikia Sh bilioni 2.8 na mapato ya msingi kwa kila hisa kuwa karibu ya Sh 45 kwa kila hisa hivyo kwa kuzingatia mafanikio hayo ndipo waliamua kupendekeza kufanyika malipo ya gawio ya Sh 17 kwa kila hisa ambayo yataokana na faida ya mwaka wa fedha wa 2021.

Kutoka kushoto Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NICOL Investment PLC, Erasto Ngamilaga akiwa kwenye picha ya maoija na viongozi wa kampuni hiyo kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa mwka wa kampuni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo  Dk. Gideon Kaunda aliwaeleza wanahisa wake kuwa kampuni imefanikiwa kukabiliana changamoto mbalimbali na kufanikiwa kushinda kesi  zaidi ya 37 ambazo zilifunguliwa dhidi ya kampuni na kuwahakikishia wanahisa kuwa kampuni hivi sasa itaendelea kutoa malipo ya gawio huku thamani ya uwekezaji wetu ikiongezaka.

Wanahisa walipendekeza kuwepo na ongezeko la idadi ya wakurugenzi wa kampuni kutoka idadi iliyopo sasa na kufikia wakurugenzi saba ili kuongeza ufanisi wake wenye kuleta tija.

Katika mkutano huo, wanahisa pia walipendekeza kuanza mchakato wa kujaza nafasi za wakurugenzi hao wapya na wakurugenzi waliomaliza muda wao kufuata taratibu za kuomba kuchaguliwa tena katika mkutano mkuu ujao.

Wanachama wa Kampuni ya Uwekezaji ya NICOLInvestment PLC wakiendelea kujisajili kabla ya kuanza kwa mkutano wao wa mwaka uliofanyika mwishoni mwa wiki

Mmoja wa wanahisa Omar Jandu alisema mwenendo wa kampuni yao ni mzuri na unataia matumaini makubwa kwani imeanza kupata faida na kutoa gawio kwa wanahisa wake.

Joseph Ulanga naye alipongeza menejiment ya kampuni hiyo kwa kuisimamia vizuri na kuwekeza kwenye miradi yenye faida hivyo kuwahakikishia kwamba itaendelea kukua na kuzalisha faida.

Habari Kubwa