Wananchi Kijiji cha Malika wajenga madarasa, ofisi

15Sep 2020
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Wananchi Kijiji cha Malika wajenga madarasa, ofisi

WANANCHI wa Kijiji cha Malika, Kata ya Malika wilayani Masasi mkoani Mtwara wameamua kujitolea kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Malika ili kupunguza adha ya baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule hiyo kusomea nje. 

Ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu katika shule ya Msingi Malika iliyopo Halmashauri ya mji Masasi mkoani, ujenzi huo unaendelea kwa kasi.PICHA HAMISI NASRI.

Hayo yalisemwa jana mjini Masasi na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Malika, Yusuph Mohamed alipokuwa akizungumza na gazeti hili, na kusema katika kijiji cha Malika kilichopo Kata ya Malika watoto wanasoma katika shule ambayo inaupungufu wa vyumba vya madarasa.

    Mohamed alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo wananchi wa kijiji hicho walikaa kikao cha Serikali ya kijiji na kutoa wazo la vijiji vyote vya kata ya hiyo vikutane na kuona namna bora ya kuisadia shule hiyo juu ya suala la kuanza ujenzi wa miundombinu yake.

   Alisema wananchi hao waliamua kuchangishana fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo viwili vya madarasa na hatimaye waliweza kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 1.7 na kwamba upatikanaji wa fedha hizo ulitokana na maazimio ya wananchi hao ya kila mwananchi mwenye nguvu ya kufanya kazi aweze kutoa Shilingi 5,000. 

 Alisema ujenzi huo tayari umeshaanza tangu Agosti mwaka huu na upo katika hatua ya msingi na kwamba wananchi hao pia wanashiriki katika hatua mbalimbali za ujenzi ikiwemo kubeba mchanga,mawe, kuchota maji na kubeba tofauti lengo likiwa ni kufanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.

  "Baada ya kukusanya fedha za michango hii walizochanga wenyewe wananchi walianza na kununua jumla ya tofari zipatazo 12,94 ambapo tofari hizo zimeshaanza kutumika katika ujenzi huo wa vyumba vya madarasa shuleni hapo," alisema Mohamed

   Alisema katika kijiji hicho kuna jumla ya wakazi 2,273 huku nguvu kazi ni 1,500 na kwamba katika idadi hiyo ya wakazi wanawake wapo 1,173 na wanaume 1,100 hivyo wananchi wamekuwa kitu kimoja katika kushirikiana kwenye shughuli za kimaendeleo.

 

John Lisombe mkazi wa kijiji hicho cha Malika alisema wameamua kujitolea kujenga vyumba hivyo vya madarasa baada ya kuguswa na watoto wanaosoma shule hiyo kusomea nje.

 Alisema wamekubaliana kila mwananchi mwenye nguvu ya kufanya kazi kutoa Shilingi 5,000 ili kufanikisha jitihada hizo za ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Naye Agnes Kasembe mkazi wa kijiji hicho, alisema wao kama wananchi wanatambua kuwa serikali inafanya mambo mengi ya kimaendeleo hivyo wananchi pia wanawajibu kusaidia jitihada hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi, Halmashauri ya Mji Masasi, Changwa Mkwazu amewapongeza wananchi hao kwa kuamua kuisadia serikali katika kuleta maendeleo.

Habari Kubwa