Wananchi wachoma moto nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji

19May 2022
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Wananchi wachoma moto nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji
  • Kisa mwenzao kupigwa risasi, ukiamuliwa ugomvi

WANANCHI wa Kitongoji namba 2 Kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga, wamechoma moto nyumba ya Mwenyekiti wa kitongoji hicho Shabani Zoro, na kuvunja nyumba ya Kiongozi wa Sugusungu, Buyaga Kazimoto na kuharibu mali zao baada ya kuwatuhumu viongozi hao kuwaonea wananchi.

Ofisi ya kitongoji Namba 2 kijiji cha Nyarigongo ikiwa imebomolewa.

 

Tuhuma hizo ni baada ya kutokea mauaji ya Jackson Joseph (35) ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini katika kitongoji hicho kuuawa kwa kupigwa risasi alipotaka kumnyang'anya bunduki mlinzi wa kampuni ya Right Security aliyekwenda kuamua ugomvi kati ya marehemu na mke wake na ndipo risasi ikamfyatukia tumboni.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari na kusema tukio la kuchomwa moto nyumba za viongozi hao na kuharibu mali zao ni baada wananchi kuutuhumu uongozi huo kukithiri kuonea wananchi na kusababisha kifo cha mwenzao.

Kyando ameeleza kuwa Mei 17 mwaka huu majira ya saa 5 usiku, marehemu Jackson alikuwa na ugomvi na mke wake Ester Emmanuel (23) na baada ya ugomvi kuwa mkubwa mwanamke huyo alikimbilia kwa jirani kuomba msaada.

Picha muonekano wa Pikipiki ya Kiongozi wa Sungusungu Buyaga Kazimoto ikiwa imechomwa Moto.

Amesema baada ya mke wake kuomba msaada, ndipo majirani wakapiga simu kwa kiongozi wa Sungusungu, Buyaga Kazimoto, ambaye naye alichukua walinzi wanne wakampuni ya ulinzi wakiwa na silaha za moto kwenda kumkamata mwanaume huyo ndipo yakatokea mauaji.

Ameeleza kuwa wakati walinzi hao kutoka kampuni binafsi ya ulinzi Light Ndovu Security, walipofika nyumbani kwa Jackson alianza kuwakimbia, ndipo mmoja wa walinzi hao Abdul Chacha alimkimbiza na alipomkamata walianza purukushani akapigwa risasi tumboni na kufariki dunia papo hapo.

Amefafanua kuwa baada ya tukio hilo la mauaji, jana Mei 18 ndipo Wananchi wa eneo hilo wakashikwa na hasira, wakidai wamechoka kuonewa na viongozi akiwamo mwenyekiti wa kitongoji na kiongozi wa Sungusungu, na kuamua kuharibu mali zao ikiwamo kuchoma moto nyumba, pikipiki na kuvunja duka na Ofisi ya kitogonji.

" Jeshi la Polisi tumashikilia mlinzi wa Kampuni ya ulinzi binafsi ya Light Ndovu Securty Abdul Chacha kwa tukio hili la mauaji ya Jacskon Joseph na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kwa hutua zaidi za kisheria,"amesema Kyando.

Habari Kubwa