Wananchi wamkataa mwekezaji mbele ya Waziri Dk. Ndumbaro

07Apr 2021
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
Wananchi wamkataa mwekezaji mbele ya Waziri Dk. Ndumbaro

WANANCHI wa vijiji 23 vilivyopo kwenye Kitalu cha Uwindaji (Lake Natron East) wilayani Longido mkoani Arusha wamemkataa mwekezaji wa kitalu hicho Kampuni ya Green Miles Safari mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro.

Wananchi hao wametaka mwekezaji huyo kusitisha shughuli zake katika eneo la Kijiji cha Lumbwa Tarafa ya Kitumbeine.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simon Oitesoi akiongozana na wananchi hao mbele ya waziri, wamedai kwa muda mrefu mwekezaji huyo amekuwa na uhusiano mbaya na jamii anayoizunguka pamoja na viongozi wa wilaya.

"Mikataba aliyosaini na vijiji hajautekeleza hata mmoja, wawekezaji ni wengi waliopo hapa hatujawahi kuingia nao kwenye migogoro kwa nini yeye tu,hatuna shida na serikali yetu sikivu bali tunashida na mwekezaji huyu" amesema Oitesoi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, amesema baada ya kufuatilia kero na madai ya wananchi hao, mwekezaji huyo alimfungulia kesi mahakamani mkuu huyo wa wilaya, na kueleza kuwa mbaya zaidi alimfungulia kesi binafsi wakati alikua akitetea maslahi ya wananchi.

"Kinachoniuma roho zaidi amenifungulia kesi binafsi mahakamani Dar- es- Salaam" ameema Mwaisumbe.

Waziri Dk. Ndumbaro, amesema leo wamefika katika eneo hilo kuwasikiliza wananchi na ifikapo Aprili 15 mwaka huu maamuzi yatatolewa na viongozi wa wilaya watashirikishwa wakiwemo pia viongozi wa Mila.

Habari Kubwa