Wananchi waondolewa hofu vifo vya Sangara

16Jan 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wananchi waondolewa hofu vifo vya Sangara

WANANCHI watakiwa kuondokana na hofu ya vifo vya samaki aina ya Sangara katika Ziwa Victoria bali waendelee na shughuli zao za kila siku ili kukuza vipato vyao na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo  yamebainishwa na Katibu Mkuu Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Rashid  Tamatamah wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini hapa, alisema mwanzoni wa mwaka huu kulitokea na taarifa ya vifo vya samaki aina ya sangara katika Ziwa Victoria nchini Uganda hasa katika maeneo ya Kasikazini Magharibi nchini humo.

Alisema baada ya tafiti zilizofanywa zimeonyesha kuwa upande wa Tanzania vifo hivyo havijaripotiwa sehemu yeyote isipokuwa kwa wavuvi na wananchi wa eneo la Masonga –Sota mkoani Tarime walidai kuona vifo vya samaki Januari 2 mwaka huu.

“Baada ya kupata taarifa hizo Wizara  ya mifugo na Uvuvi ikishirikiana na Taasisi yake ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kituo cha Mwanza iliwasiliana na maofisa uvuvi,wavuvi,na wadau wengine wa uvuvi katika Ziwa Victoria ikiwemo chama cha wavuvi( TAFU)  na tulibaini hakukuwa na taarifa za vifo “alisema Tamatamah.

Alisema katika kufuatilia suala hilo waliwasiliana na Idara ya Uvuvi ya Uganda ambao walitoa taarifa ya kuwa walipeleka sampuli za samaki waliokufa katika maabara mbalimbali nchini mwao ili kujua kama kuna maambukizi ya sumu ya aina yeyote inayosababisha vifo vya samaki hao.

“Idara hiyo imeweza kutuhakikishia kuwa samaki hawakuwa na sumu na inadhaniwa kuwa vifo hivyo vimetokana na tukio la kila mwaka linalotokana na mchanganyiko wa maji ziwani kati ya tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni na lile tabaka la juu”alisema

Akielezea hali ya ziwa hilo katika  mzunguko wa majira ya mwaka husababisha matukio mawili ambayo ni utengenezaji wa matabaka ya maji kati ya tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni na lile tabaka la juu lenye hewa ya Oksijeni ya kutosha  linatokea kuanzia Januari hadi Aprili ambapo ni kipindi cha mvua kubwa lingine ni mchanganyiko wa maji  kati ya tabaka la juu na chini ambalo hutokea wakati wa kiangazi na upepoi mkubwa  kuanzia Juni hadi Septemba.

Alisema katika hali ya kawaida Sangara huishi katika maji ya tabaka la kati na juu kuanzia 15m hadi 20m ambalo lina hewa ya kutosha ya Oksijeni zaidi ya miligranu 3 kwa lita.

Aliongeza kuwa wakati wa kipindi cha mchanganyiko wa maji kutoka tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni hupunguza kiwango cha hewa  hiyo chini ya miligranu 3 kwa lita katika tabaka la kati na juu wanakoishi Sangara hivyo chini ya kiwango hicho cha hewa samaki hao hasa wakubwa hushindwa kuvumilia na kufa hali hiyo hutokea kila mwaka au kila baada ya miaka michache.

“Pamoja na kuwa vifo hivyo havijaonekana kwenye maji ya upande wa Tanzania ,kuna uwezekano  kuwa mchanganyiko wa maji unaweza kutokea kwetu pia kama hali ya hewa itaruhusu wakati wa mvua kubwa na upepo mkubwa hivyo Wizara na wadau wa sekta ya uvuvi wanaendelea kufuatilia uwezekano wa kujitokeza vifo hivyo”alieleza

Aidha aliongeza kuwa pale vitakapojitokeza hatua za haraka zitachukuliwa ili kubaini kama vinasababishwa na chanzo kilichozoeleka cha mabadiliko ya hali ya ziwa au vinatokana na shughuli za kibinadamu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema. 

Habari Kubwa