Wananchi, mbunge kujenga kituo cha polisi

25Jan 2021
Dinna Stephano
Tarime
Nipashe
Wananchi, mbunge kujenga kituo cha polisi

WANANCHI wa kata ya Itiryo, wilayani Tarime mkoani Mara kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara, wamechanga fedha ili kujenga kituo cha polisi kwa lengo la kuimarisha ulinzi na kupambana na uhalifu.

Baadhi ya matukio ya uhalifu yamedaiwa kufanywa na watu wa nchi jirani kwa kushirikiana na baadhi ya Watanzania wanaoishi mpakani.

Waitara akizungumzia suala la ulinzi na usalama katika maeneo ya mipakani, alisema anachukizwa na vitendo vya mauaji na uhalifu vikiwamo vya watumishi wa serikali kuvamiwa na kuporwa fedha na mali.

"Tukio la mwalimu kuuawa liliteta taswira mbaya na nilitumia nguvu nyingi kulishughulikia, lakini bado watu hawasikii wanaendelea na vitendo vya uhalifu na kuchukua mali za watu, kuna mwananchi wa kijiji cha Itiryo alipigwa risasi akafa, na inaelezwa kuwa majambazi wanatoka nchi jirani ya Kenya na wanashirikiana na wahalifu kutoka kata ya Itiryo," alisema Waitara.

Waitara alisema matukio ya kihalifu yamezidi kuleta hofu kwa watumishi wa serikali wakiwamo walimu wa shule ya msingi kata ya Itiryo huku baadhi yao wakiomba uhamisho ili kunusuru maisha yao jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma taaluma ya wanafunzi.

"Nimeambiwa kuwa kuna walimu wanataka kuhama matukio kama haya yanashusha heshima ya kabila letu la Wakurya na ndiyo maana tunachukuliwa kama ni watu wakorofi, kwanini tuwafiche wahalifu, lazima tuwataje kwa njia zozote hata kama ni kwa siri ili wakamatwe tukiyaacha haya maovu watu watahama kata na uchumi utashuka, kwa kuwa mmekubali kituo kijengwe nachangia milioni tano ya ujenzi, " alisema Waitara.

Nchagwa Matare, alisema suala la kujengwa kituo cha polisi lilishazungumzwa na kuna maeneo ambayo yanaweza kutumika kukijenga na kuwaomba viongozi wa serikali za vijiji kuhamasisha wananchi kuchangia fedha na nguvu kazi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Itiryo, Chacha Paulo, aliwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati viongozi wa serikali wakitafuta ufumbuzi wa suala la uhalifu katika maeneo hayo.

Habari Kubwa