Wananchi wahimizwa kuchanja ili kulinda afya

15Sep 2021
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wananchi wahimizwa kuchanja ili kulinda afya

WATAALAMU wa afya wemeendelea kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanapata chanjo ya UVIKO-19 ili kulinda afya zao kwani chanjo ni salama na zinasaidia kuondokana na hali ya hatari pindi mtu anapopata ugonjwa huo.

Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo kikuu cha Uuguzi cha Rheumatology (University of the West of England, Bristol) Dk. Mwidini Ndosi.

Hayo yalisemwa na Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo kikuu cha Uuguzi cha Rheumatology (University of the West of England, Bristol) Dk. Mwidini Ndosi alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Internews Tanzania na ulihusisha wadau wa afya na wanahabari, ambapo ulifanyika mwanzoni mwa wiki hii kwa njia ya mtandao (zoom).

Alisema tafiti mbalimbali zilizofanyika ili kubaini ufanisi wa chanjo zilizopo ikiwemo Johnson & Johnson, Moderna, Pfizer-BioNTech na Oxford-AstraZeneca. Kwa asilimia kubwa zilionyesha kuwa ni salama na huleta unafuu na matokeo chanya kwa mtumiaji dhidi ya UVIKO-19.

“Kunawatu wanauelewa hafifu juu ya elimu ya chanjo ya UVIKO-19, serikali katika baadhi ya nchi za ulaya na sehemu nyingine ziliwekeza sana katika suala la uelimishaji kwani watu ili waitumie ni lazima waelimishwe ili waweze kuielewa ndo waitumie. Pia wataalamu wa afya wanatakiwa kupewa uelewa juu ya chanyo hizo ili watoe huduma yenye ufanisi,” alisema Dk Ndosi.

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya taarifa zinasambaa kutokana na matokeo ya chanjo hizo, na alikanusha kwamba si kweli kuwa baadhi ya kinga hizo zinasababisha ongezeko la nguvu za kiume na alidai kuwa hazina madhara yeyote kwenye suala hilo.

Pia alisema kuhusu mabadiliko yanayotajwa kujitokeza baada ya kutumia chanjo hizo kwa upande wa wanawake katika mzunguko wa hedhi ni jambo lililoongelewa sana lakini katika utafiti na wakati wa majaribio haikuonekana kuwa iliwaathiri.

Alisema matokeo ya tafiti kwa waliotumia chanjo zenje dozi mbili kwa wale wenye umri wa miaka 80 na kuendelea, jumla ya watu 156,930 wenye chanjo, kati yao waliopata UVIKO-19 ni 44,590 sawa na asilimia 28.4, na wasiopata ni 112,340 sawa na asilimia 71.6.

“Ufanisi wa dozi hizo ni asilimia 70 kwa ndani ya siku 28-34 baada ya kupata chanjo ya kwanza, na asilimia 89 ndani ya siku 14 baada ya kupata chanjo ya pili.

“Lengo la tafiti ni kujua uwezekano wa kupata maambukizi kati ya watu waliopata chanjo ya Johnson & Johnson na wasiochanjwa, na matokeo tangu Februari 27 hadi Aprili 14 mwaka huu, kati ya kundi la wale waliochanjwa 17,744, waliopata maambukizi ni 128 sawa na asilimia 0.72. Kati ya watu 1,779 waliochanjwa na kufuatiliwa baada ya wiki mbili waliopata maambukizi ni watatu tu, sawa na asilimia 0.17,” alisema Dk Ndosi.

Pia alieleza kuwa kwa mujibu wa takwimu hizo ni wasa kuwa uwezekanao wa maambukizi umepunguzwa kwa zaidi ya mara 4.34, huku ufanisi halisia wa chanjo ukitajwa kuwa ni zaidi ya asilimia 76.7 katika kuzuia maambukizi, na alibainisha kwamba waliochanjwa hubaki na kinga ya ziada kwa zaidi ya asilimia 51 ya kuzuia ugonjwa mkali na kulazwa pamoja na vifo .

Aidha katika baadhi ya maeneo watu huonekana kutotilia maanani tahadhari juu ya janga la Corona, huku wengi katika vyombo vya usafiri vya umma kwa asilimia kubwa wakiwa hawajavalia Barakoa hali inayoruhusu kupumuliana, jambo ambalo si salama na huweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa huo.

“Si kweli kuwa watu wanakufa kwa hofu ya UVIKO-19 ila watu wanakufa wanapoumwa wakiwa wanasubiri oxgen, na endapo hakutakuwa na tahadhari ya ugonjwa kunaweza kukawa na kirusi kingine. Kuchukua tahadhari ni muhimu hatutaki Tanzania kukawa na kirusi kingine.

“Hivyo watu wachanje ugonjwa huu ni hatari, chanjo ni sehemu kubwa ya ufumbuzi, pia ni salama, huzuia ugonjwa mkali na vifo. Pia waandishi wa habari wafuatilie habari za kisayansi zinazohusu UVIKO-19 kuwa zinatoka wapi ili hata wanapozisambaza ziwe na uhakika,” alishauri Dk Ndosi.

Habari Kubwa