Wananchi walalamika watu waliotafuna fedha za serikali

27Feb 2021
Gurian Adolf
Sumbawanga
Nipashe
Wananchi walalamika watu waliotafuna fedha za serikali

BAADHI ya wananchi mkoani Rukwa wamesikitishwa na kitendo cha kutochukuliwa hatua mpaka sasa baadhi ya watendaji  wa serikali wanaotuhumiwa kula fedha za makusanyo ya mapato ya halmashauri, hali waliyodai inawakatisha tamaa kulipa tozo na kodi mbalimbali.

Wananchi hao walisema hayo juzi, kwa nyakati tofauti baada ya kusikia Mkuu wa Mkoa huo, Joachim Wangabo, ametoa siku 14 wawe wamerudisha Sh. milioni 932 vinginevyo watafikishwa mahakamani.

Mmoja wa wananchi hao, Furaha Kabinda, mkazi wa wilayani Nkasi, alisema anasikitika kuona watuhumiwa hao hawajafikishwa mahakamani ili wakajibu tuhuma dhidi yao.

"Nimeshtuka sana kusikia suala hili kama bado halijaisha, maana tangu nimeanza kulisikia ni zaidi ya mwaka sasa. Kitendo hiki ni kucheza na maendeleo ya wananchi, sisi tunalipa kodi ili tupate maendeleo, baadhi ya watendaji wa serikali wanakula fedha hizo. Huku ni kucheza na maisha yetu," alisema.

Naye Flaviana Kilosa, mkazi wa Sumbawanga Mjini, alisema kitendo hicho kimemsikitisha kwa kuwa watuhumiwa wa wezi walioko mitaani wanakamatwa na kufikishwa mahakamani haraka, lakini watendaji wa serikali wanabembelezwa kurejesha fedha za umma hii si sawa.

"Pamoja na kuwa watuhumiwa hao wamefikishwa TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) walipaswa wafikishwe mahakamani upesi ili wananchi tuone hatua zinachukuliwa haraka kwani kumekuwapo na hisia kwa kuwa ni mali ya umma ndiyo maana kuna kusuasua na hii inawakatisha tamaa walipakodi," alisema.

Hivi karibuni, Wangabo alitoa siku 14 kwa watendaji wa serikali na watu waliokuwa mawakala wa kukusanya mapato katika halmashauri zote nne za mkoa huo wanaodaiwa kula fedha mbichi za serikali, wazirejeshe vinginevyo atawaagiza TAKUKURU kuwafikisha mahakamani.

Alisema mkoa huo uliweka makisio ya kukusanya Sh. 9,487,289,000 katika mwaka wa fedha wa 2020/21, lakini mpaka nusu ya kwanza ya mwaka, umekusanya Sh. 3,682,531,918.16, sawa na asilimia 38.8 tu.

Habari Kubwa