Wananchi waombwa kumuombea Magufuli

21Mar 2021
Hamisi Nasiri
MASASI
Nipashe Jumapili
Wananchi waombwa kumuombea Magufuli

MKUU wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara,, Selemani Mzee amewaomba wakazi wa wilaya hiyo kufanya maombi ya heshima ya kumuombea aliyekuwa Rais Dk.John Magufuli kwa lengo la kumkumbuka na kumuenzi kwa mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake.

Mzee, aliyasema hayo mara baada ya kusaini kitabu cha kumbukumbuku ya maombolezo ya Dk.Magufuli.

Amesema anafahamu kuwa wananchi wa wilaya yake wamesikitishwa na kifo cha Dk.Magufuli kwa vile bado wanamasasi walitamani kuendelea kuwa nae ili aweze kufanya mambo mengine mbalimbali ya kimaendeleo kwa ajili ya manufaa ya taifa na kizazi kijacho.

Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa wilaya ya Masasi itamkumbuka Rais Dk. Magufuli kwa kutambua mambo mengi ya kimaendeleo aliyoyafanya wakati wa uhai wake ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya maji, vyumba vya madarasa na miundombinu ya barabara.

Amesema kupitia miradi mikubwa ya kimaendeleo iliyofanyika wilayani Masasi katika kipindi cha uhai wake hakuba budi kwa wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kumuhenzi kwa yale yote aliyoyafanya kwa kila mmoja kufanya maombi kwa ajili ya kuyahenzi mazuri aliyoyafanya ndani ya wilaya ya Masasi.

 

Habari Kubwa