Wananchi watahadharishwa kasi maambukizi ya matende, mishipa

03Sep 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Wananchi watahadharishwa kasi maambukizi ya matende, mishipa

WANAUME takribani milioni 4.7 nchini wanaweza kupatwa na maambukizi ya ugonjwa wa mshipa (busha) na matende kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa mbu wanaosambaza maradhi hayo.

Hayo yalisemwa juzi na Afisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) Osca Kaitaba, wakati wa kutoa dawa za matende na mabusha kwa wananchi wa Muheza.

Alisema watu pia wanaweza kupatwa na maambukizi ya ugonjwa wa mabusha, kichocho na minyoo na kwamba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inaanza kupunguza tatizo hilo la magonjwa hayo ambayo pia ni hatari.

Kaitaba alisema ugonjwa wa trakoma au vikope unaoshambulia macho takribani watu milioni 12.5 wameathirika wakati usubi unaoharibu ngozi unaweza kuathiri watu milioni sita.

“Tunajitahidi kuhakikisha tunadhibiti magonjwa hayo kwa haraka kwa kusambaza dawa kila wilaya nchini.”

Alisema kuwa halmashauri 47 nchini zimetokomeza ugonjwa wa trakoma wakati 58 zimetokemeza mabusha na kwamba
lengo ni kuondoa magonjwa hayo kwa asilimia 90 kwa kupeleka dawa wilaya zote.

Kwa upande wake Mfamasia wa hospitali ya Bombo mkoa wa Tanga John Mmasi, alisema wameanza kutoa chanjo ya matende
na mabusha katika mkoa wa Tanga hususani wilaya ya Muheza lakini wanashindwa kuwafikia wananchi wote huko vijijini kutokana na ugumu wa usafiri.

Alimuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza Luiza Mlelwa, kutoa usafiri ili kufikia watu wote wa vijijini.

Kwa upande wake Mlelwa alisema kuwa fedha za kuendesha huduma hizo zimetolewa na kwamba lazima watu wote watafikiwa kupewa dawa hizo za matende na mabusha katika wilaya hiyo hata wale wanaotaka kufanyiwa upasuaji wa mabusha watahudumiwa, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Matthew Mganga, alisema kazi hiyo ya ugawaji dawa za matende na mabusha watalisimamia kikamilifu ili kuhakikisha kila mwananchi anapata dawa hizo za matende na mabusha.

Habari Kubwa