Wananchi watakiwa kuheshimu haki ya msingi afya ya uzazi

07Aug 2019
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
Wananchi watakiwa kuheshimu haki ya msingi afya ya uzazi

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa  linalohusika  na Idadi ya Watu na Maendeleo (UNFPA ) limewataka wananchi kutambua kuwa afya ya uzazi ni haki ya msingi kwa kila mtu hivyo ni vema ikaheshimiwa.

mratibu wa UNFPA Mkoa wa Simiyu Dk. Amir Batenda akitoa maelezo juu ya shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

Hayo yamesemwa leo na Mratibu wa shirika hilo Mkoa wa Simiyu Dk.  Amir Batenga, wakati akitoa elimu kwa  wananchi waliotembelea banda lao  lililopo katika viwanja  vya  maonesho ya nane nane Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Dk. Batenda amesema kuwa shirika lao  kwa kutambua hilo wamejikita kusaidia kuyafikia malengo endelevu  makuu matatu ambayo ni kupunguza vifo vya akinamama, ukatili wa kijinsia, mimba za utotoni, ukeketaji pamoja na kusimamia haki ya msingi ya uzazi.

Amesema watu wengi wamekuwa na uelewa tofauti juu ya haki ya afya ya uzazi na kupelekea baadhi ya mataifa kuwapangia wananchi wake idadi ya watoto wanaopaswa kuwa nao wakati ni kinyume na haki ya msingi ya afya ya uzazi.

Ameongeza kuwa hilo si sawa na wao kupitia malengo makuu ya kumlinda mwanamke na mtoto wa kike yameeleza na yanatambua kuwa mtu mwenyewe ndiye anayepaswa kuchagua na kuamua idadi ya watoto anaotaka kuwa nao.

Dk. Batenga ameongeza kuwa UNFPA wanasaidia kuhakikisha wanasimamia yote hayo pamoja na kuweka miundombinu rafiki ya afya na kutoa elimu kwa wote ili kupunguza vifo vya akinamama na mimba za utotoni.

Amesema  toka kupitishwa kwa  maadhimio makuu ya kimataifa  mwaka 1994 ni miaka 25 sasa imepita na kumekuwepo na mafanikio makubwa sana kwani vifo vya akinamama,mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia vimepungua.

Pamoja na mafanikio hayo amewaomba wananchi wa Simiyu na wa Mikoa mingine kuungana kwa pamoja kusimamia haki hizo zinatetewa na kutekelezwa.

Habari Kubwa