Wananchi watakiwa kutumia huduma za kidigitali za Shirika la Posta

21Oct 2021
Woinde Shizza
Arusha
Nipashe
Wananchi watakiwa kutumia huduma za kidigitali za Shirika la Posta

​​​​​​​SHIRIKA la Posta Tanzania mkoani Arusha limewataka wananchi kutumia huduma za kidigitali zinazotolewa na shirika hilo ambalo limerahisisha utoaji wa huduma zake kuwa za kisasa na haraka zaidi.

Meneja wa Posta Mikoa ya Manyara na Arusha Athuman Msilikale akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa wadau wa Tehama unaofanyika mkoani Arusha Katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa AICC.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Posta Mkoa wa Arusha na Manyara Athuman Msilikale, wakati akizungumza katika mkutano wa tano wa wadau wa Tehama unaoendelea mkoani Arusha.

Amesema kuwa, hivi sasa shirika hilo limebadilisha utoaji huduma zake kutoka analojia kwenda digitali zaidi ambapo mifumo hiyo ya kidigitali inawarahisishia wateja kuweza kupata huduma kwa haraka .

Msilikale amesema kuwa,shirika hilo limeweza kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo ya biashara mtandaoni,huduma za kiganjani,huduma za Posta mlangoni,huduma za EMS ,huduma za barua za kawaida na huduma ya wateja wakiwa na bidhaa zao,pamoja na huduma za Posta Cargo ambapo huduma zote hizo zinawasaidia wateja kupata huduma kwa haraka na popote pale walipo.

"Sasa tumefikia hatua ya kutumia mifumo ya Tehama na wananchi wameweza kuelewa vzuri mifumo hii hasa katika soko na kuweza kutangaza bidhaa zetu kwa njia ya mtandao na hatimaye kuweza kukuza soko la ajira ndani na nje ya nchi" amesema.

Aidha, amefafanua kuwa, shirika hilo limeweza kuboresha huduma zake kwa kutoa huduma kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa hali ambayo imewezesha Serikali kuendelea kupata kodi.

Hata hivyo ametoa wito kwa wadau, wananchi, Taasisi pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kuhakikisha wanalitumia shirika hilo katika kupata huduma mbalimbali kwa kutumia mifumo ya Tehama ambayo imeboreshwa zaidi.

Habari Kubwa