Wanane wafariki dunia kwenye ajali

24Nov 2020
Restuta Damian
Bukoba
Nipashe
Wanane wafariki dunia kwenye ajali

WATU​ wanane​ wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari yenye namba za usajili T.471 DGC, Toyota Hiace inayofanya safari zake kati ya Kemondo wilayani Bukoba kwenda Bukoba mjini mkoani Kagera, kupoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye shimo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi, alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kufunga breki na kuparamia watembea kwa miguu.

Wakizungumza​ na Nipashe eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda walisema baada ya gari hiyo kupoteza mwelekeo liliwagonga watu hao.

Shuhuda Riclain Ndostaini, alisema alikuwa barabarani kuelekea nyumbani na kushuhudia mama mmoja akivuka barabara kupisha gari hilo, lililokuwa likiendeshwa kwa kasi ambalo lilimgonga na kufariki dunia papo hapo.

"Mama huyo alikuwa akitokea maeneo ya sokoni wakati anavuka barabara nikaona anagongwa na gari hilo. Mwili ulikuwa unaburuzwa na ndani ya gari walikuwa watu wanne ambao tumewaokoa mmoja alikuwa ameshakufa, mwingine ameumia mkono mmoja ameangukia shimoni," alisema Ndostaini.

Mganga aliyepokea majeruhi wa ajali hiyo, Dk. Yustas Tibanga, alisema walipokea marehemu sita na majeruhi wanane.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi, alisema, tukio hilo lilitokea Novemba 22, saa 2:00 usiku eneo la​ Kata ya Rwamishenye, Manispaa ya Bukoba.

"Dereva Ismail Rashid (37), mkazi Kemondo ni majeruhi, lakini atakuwa chini ya ulinzi ili taratibu nyingine ziweze kufuatwa baada ya kupatiwa matibabu kwani alikuwa mwendo kasi na kusababisha ajali kubwa kama hii ambayo ni ya pili kutokea kwa matukio ya ajali ya kupoteza watu," alisema Malimi.

Malimi alisema, baada ya dereva huyo kuona hitilafu imetokea na kushindwa kulimudu gari, alilishusha kwenye mteremko mkali ng'ambo ya barabara ambako kuna shimo na kutumbukia.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Charels Kahigi, alisema vifo vingine vimeongezeka kutoka watu sita hadi wanane na majeruhi sita.

Alitaja majina ya marehemu waliotambuliwa kuwa ni Rausati Khalfan (35), Rehema Abubakari (30), Jonson John (26), Anchila Rweyendele (62) na Retisia Grayson (58), Dominick Kibuka (48).

Alitaja majeruhi wanaondelea kupata matibabu kuwa ni Bahati Alex (22), Johaness Gilbert (20), Shila Maurd (28), Vedasto Likera (22), mwingine aliyetambulika kwa jina moja Projestus (20), Roda Johnbosco (20) na Mecktrida Andikile (19).

Habari Kubwa