Wanaoambukizwa Ukimwi kwa makusudi kulipwa fidia

13Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Wanaoambukizwa Ukimwi kwa makusudi kulipwa fidia

BUNGE limefanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, ambapo pamoja na mambo mengine imeipa mamlaka Mahakama kutoa amri ya fidia kwa mtu aliyeambukizwa VVU kwa makusudi.

Pia, limepitisha umri wa mtoto kujipima VVU ni 15, huku wabunge wa upinzani wakitaka iwe miaka 12.

Awali akiwasilisha muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adelardus Kilangi, alisema inapendekezwa kufanya marekebisho kwa lengo la kujumuisha katika sheria hiyo masharti ya kujipima VVU.

Prof. Kilangi alisema marekebisho hayo yanalenga kuainisha wajibu kwa mtu anayejipima VVU na mtu anayetoa au kusambaza vifaa vya kujipima VVU na kumuwezesha Waziri kutoa miongozo ili kuhakikisha kuna usimamizi wa viwango vya vifaa vya kujipimia VVU vinavyosambazwa au kuuzwa kwa watumiaji.

Alisema muswada huo pia umependekeza kuweka wajibu wa kutunza siri kwa mtu anayemsaidia mtu mwingine kujipima na kufanya kitendo cha kutoa siri kuwa kosa chini ya sheria hiyo.

Alisema marekebisho hayo yamelenga kuweka bayana umri wa mtoto katika masuala ya upimaji wa VVU na kueleza maana ya dhana ya kujipima VVU.

Prof. Kilangi alisema marekebisho hayo pia yanalenga kuwezesha vituo vyote vya huduma ya afya kutoa huduma ya upimaji, bila kujali kuwa vituo hivyo ni vya umma au vya watu binafsi.

”Inapendekezwa kurekebishwa kwa lengo la kuruhusu majibu ya vipimo ya mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 kutolewa pia kwa mzazi, mlezi au mtu mwingine ambaye mwenye vipimo anamuamini. Pia inapendekeza kurekebisha kumpa Waziri mamlaka ya kutengeneza Kanuni za utoaji, usambazaji, matumizi na utupaji wa vifaa vya kujipimia VVU,” alisema Prof. Kilangi.

Alisema kifungu cha 23(2) kinarekebishwa ili kuhakikisha kuwa kondomu zinazotengenezwa au kuingizwa nchini zinaidhinishwa na mamlaka zinazohusika na udhibiti wa viwango Tanzania, bila kuwa na haja ya kuzitaja mamlaka hizo kwa majina.

Alisema Kifungu cha 27(3) kinarekebishwa kwa dhumuni la kuongeza adhabu kwa kosa la kutoa taarifa za kupotosha kuhusu tiba au udhibiti wa VVU na Ukimwi.

Prof. Kilangi aliseman marekebisho hayo yanalenga kuzuia watu kutoa matamko kuhusu tiba ya Ukimwi bila ushahidi wa kisayansi.
Mbunge wa viti maalum Chadema, Suzan Lyimo, alisema mkoani Shinyanga asilimia 50 ya watoto wanaopata ujauzito wana umri chini ya miaka 18.

Alisema kigezo cha mtoto kujipima VVU iwe kuanzia miaka 12 na siyo 15 kwani umri huo ni sahihi.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh, alisema endapo watoto kuanzia umri wa miaka 12 hadi 14 wakiachwa bila ya kupimwa VVU taifa litakuwa linatengeneza bomu watapofikisha miaka 15.

Akitolea ufafanuzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema lengo la kuweka umri wa miaka 15 kutokomeza maambukizi ya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Alisema lengo la serikali ifikapo mwaka 2020 ni fikikia 90, 90, 90, lakini changamoto kubwa ni kuifikia 90 ya kwanza ambayo ni kuhakikisha kila Mtanzania awe amejua hali yake ya maambukizi.

Habari Kubwa