Wanaochungisha watoto mifugo wapewa kibano

20Jul 2019
Cynthia Mwilolezi
MANYARA
Nipashe
Wanaochungisha watoto mifugo wapewa kibano

VIONGOZI wa kimila wa jamii ya wafugaji (malaigwanani) wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamepitisha sheria ndogo ya kuwatoza
Sh.milioni moja watakaochungisha mifugo watoto wao badala ya kuwasomesha.

Sheria hiyo pia inawabana wazazi ambao wanashiriki katika vitendo vya kuwakeketa watoto wao wa kike.

Wazee hao wa kimila waliyasema hayo wakati wakizungumza jana mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, kwenye sherehe za kimila Kijiji cha Lengast Kata ya Naisinyai.

Meibuko Parasoi, alisema wamelenga kuhakikisha mila zilizopitwa na wakati wanaachana nazo na mtu ambaye hatatimiza makubaliano hayo, atatozwa faini hiyo.

Parasoi alisema kwa sababu rasilimali kubwa ya jamii ya wafugaji ni mifugo, wameazimia kuwapa elimu watoto wao ili waendeleze ufugaji wenye tija na kuachana na ukeketaji kwa wasichana.

Chaula aliwapongeza viongozi hao wa kimila kwa kuweka mikakati hiyo ya kupambania vijana wao wasome na kumaliza vitendo vya kikatili vya ukeketaji wasichana.

Chaula alisema wale wanaokeketa wasichana wanapaswa kutambua kuwa suala hilo limepitwa na wakati na hivi sasa linaitwa ‘zilipendwa’ kwani jamii imestaarabika na kuachana nayo.

“Watoto wa kike wanasomeshwa, watoto wa kiume wanasomeshwa wote wana haki sawa, pia Malaigwanani mkemee wasichana kupata mimba shuleni na kuolewa wakiwa wadogo,” alisema.

Mmoja kati ya wakazi wa kijiji cha Lengast, Elias John, alisema anaunga mkono hatua hiyo kwa sababu bila kuweka faini hiyo vitendo vya ukeketaji na kusomesha watoto wao havitadhibitiwa.

"Wengine wamekuwa wanakeketa watoto wao kwa kisingizio cha kuwa na ugonjwa wa fangasi ukeni maarufu kama ‘lawalawa’, lakini wanapaswa kuwapeleka hospitali na siyo kuwakeketa,” alisema John.

Mkazi wa kijiji cha Lengast, Esupati Mollel, alisema ili kutimiza hayo, Jamii pia ipatiwe elimu na kukubali kubadilika kwa lengo la kwenda na wakati na kuachana na mila kandamizi zisizo na mashiko.

“Sisi wanawake tunaunga mkono suala hilo japokuwa tunaona kutumia sheria ndogo siyo vizuri tofauti na elimu kutolewa na jamii kuacha wenyewe ukeketaji wa wasichana na kuwapeleka shule vijana badala ya kuchungisha mifugo,” alisema.

 

Habari Kubwa