Wanaoharibu majengo makumbusho waonywa

24Jul 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
Wanaoharibu majengo makumbusho waonywa

SERIKALI amewaonya wananchi wanaokaa katika majengo mbalimbali ya makumbusho kuacha kuharibu uhalisia wa miundombinu hiyo kwa dhamira ya kubadilisha mwonekano wa asili.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja,  alitoa onyo hilo jana katika eneo la Makumbusho ya Malikale ya Mikindani, mkoani hapa akiwa kwenye ziara ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kuangalia namna ya kuboresha pasipo kuharibu uhalisia wake.

Alisema kubadilisha uhalisia wa majengo hayo yanayotambulika kama malikale ni sawa na kudhulumu haki ya vizazi vijavyo kutojua wapi nchi yao imetoka na inakokwenda kwa kuwa hakutakuwa na ushahidi wowote wa kuonyesha uhalisia wa nyuma.

Masanja alisema lengo la wizara ni kuona eneo la Mikindani linatambulika kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuwavutia watalii wengi na kuwashukuru wakazi wa Mikindani kuendelea kutunza majengo ya kale pasipo kuharibu uhalisia wake.

“Kuna maeneo tumegundua wakazi wa kwenye majengo ya makumbusho wanayaharibu makusudi ili wapate nafasi ya kujenga majengo ya kisasa pasipo kupata utaratibu wa namna ya kutunza kumbukumbu iliyopo. Hilo hatutaliruhusu, alisema.

Alisema ni ngumu kuwavutia watalii ikiwa maeneo ya kale yatapoteza uhalisia wake na kuagiza Idara ya Makumbusho ya Taifa kuanza kuweka vyakula vya asili katika maeneo hayo kwa ajili ya kutoa fursa kwa wageni kujifunza utamaduni wa wenyeji yakiwamo mapishi.

Pia alitumia ziara hiyo kumjulia hali Mzee Hassan Kidume, anayetajwa kuwa mwenyeji wa Mwalimu Julius Nyerere katika maeneo hayo ya Mikindani mwaka 1954 alipokuwa katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Awali, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Noel Luoga, alsiema idara  imeshaandaa mwongozo wa namna ya kukarabati majengo yote ya makumbusho na kwa sasa wanatarajia kuifikisha kwa wadau Agosti 5, mwaka huu.

Habari Kubwa