Wanaojiunga kidato cha tano, vyuo vya ufundi ruksa kubadili tahasusi

25Mar 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Wanaojiunga kidato cha tano, vyuo vya ufundi ruksa kubadili tahasusi

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imetangaza fursa ya wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kubadili tahasusi au kozi wanazotaka kusomea kabla ya kuchaguliwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo.

Katika uchaguzi huo, wanafunzi 135,301 wenye ufaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu ambao walihitimu kidato cha nne mwaka 2019 wanatarajiwa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo amesema wanafunzi hao watabadili tahasusi na kozi kwa njia ya mtandao kuanzia leo hadi Aprili 19, mwaka huu.

Amesema utoaji wa fursa ya kufanya mabadiliko kwenye tahasusi na kozi umetokana na baadhi ya wanafunzi kutojaza kwa uhakika tahasusi zao kwa kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo yao.

Amebainisha kuwa wanafunzi hao watakuwa na uwezo wa kubadili machaguo au kuchagua kutoka kidato cha tano kwenda Chuo au Chuo kwenda kidato cha tano.

Jafo amefafanua kuwa hatua hiyo inatoa mwanya kwa mwanafunzi kusoma fani itakayomwandaa kuwa na utaalam fulani katika maisha yake ya baadaye kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauriwa na wazazi au walezi wake.

“Mabadiliko haya yanafanyika kupitia mtandao kwenye anuani selform.tamisemi.go.tz , ikitokea hadi baada ya Aprili 19 mwaka 2020 mwanafunzi hajabadili Tahasusi maana yake chaguo lake la awali ndo hilo hilo hatutaki kuona malalamiko yeyote,”amesema.

Habari Kubwa