Wanaokwenda China kuchukuliwa alama za vidole

13Feb 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaokwenda China kuchukuliwa alama za vidole

WIZARA ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema Ubalozi wa China nchini Tanzania imeanzisha mfumo wa kuchukua alama za vidole kwa waombaji Visa.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Emmanuel Bohohela.

Taarifa hiyo ilisema kutokana na kuanzishwa kwa mfumo huo Desemba 24, mwaka jana, mwombaji atalazimika kufika ofisi ya ubalozi huo ili kuchukuliwa alama za vidole kama sehemu ya kukamilisha taarifa za uombaji wa visa.

“Ubalozi umeeleza kuwa utaratibu huu hautawahusu waombaji walio katika makundi ambayo ni wenye umri chini ya miaka 14 na zaidi ya miaka 70.

“Wengine ni waombaji wenye pasi za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi, waombaji walioomba visa kwa kutumia pasi ya awali ambayo tayari alama za vidole zilichukuliwa na haijamaliza muda wa miaka mitano,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilitaja makundi mengine ambayo hayatahusika kuwa ni wale wenye matatizo ya alama za vidole katika vidole vyote 10 vya mikono au vyote vyenye ulemavu ambao hautawezesha alama za vidole kuchukuliwa.

“Serikali ya China inaendelea kuboresha taratibu za mifumo ili kuwezesha mwingiliano wa China na mataifa mengine na inawakaribisha wageni wote kutembelea nchi hiyo,” ilisema taarifa hiyo.

Habari Kubwa