Wanaomiliki hati zinazoishia miaka 33 waitwa kupewa za miaka 99

05Jul 2020
Dotto Lameck
Mara
Nipashe
Wanaomiliki hati zinazoishia miaka 33 waitwa kupewa za miaka 99

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewataka wamiliki wa ardhi wenye hati zinazoishia miaka 33 kufika katika ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni kuzipeleka ili wapatiwe za miaka 99.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Mara wakati akizindua Ofisi ya ardhi mkoani humo ambayo ni ofisi ya kumi na mbili kuzinduliwa ikiwa ni mfululizo wa kuzindua ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Lukuvi amesema, kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi kwenye mikoa mbalimbali ambao viwanja vyao vimepimwa na michoro kuidhinishwa lakini hati zao ni za miaka 33 hivyo wanatakiwa kwenda katika ofisi husika kubadilishiwa ili wapatiwe za miaka 99.

“Hati nyingi za wale wamiliki ambao hawajazichukua zimekwisha muda wake, muende kwenye ofisi za ardhi za mikoa, huko mtaelekezwa na wasajili wasaidzi wa ardhi katika ofisi hizo namna ya kuzibadilisha ili mpatiwe za miaka 99’’ amesema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi,  amewataka zaidi ya wamiliki wa ardhi 50,000 mkoani Mara hawajachukua hati za ardhi na wengine muda wa hati zao unaishia miaka 33 kufika ofisi za ardhi mkoani humo kurekebishiwa na kupatiwa za miaka 99 ili iwe rahisi kupata mikopo mikubwa .

Akizungumzia uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Mara, Lukuvi amesema Mkoa huo umekuwa na migogoro mingi ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo utawawezesha wananchi wa Mara kumaliza migogoro kupitia ofisi hiyo badala ya kuipeleka migogoro kwake.

Habari Kubwa