Wanaomiliki visima vya maji ilala waonywa

06Mar 2017
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaomiliki visima vya maji ilala waonywa

SHIRIKA la Majisafi na Majitaka (DAWASCO), limesema liko kwenye hatua za mwisho kuanza mpango wa kuwaunganisha wamiliki wa visima binafsi vya maji kwenye mtandao rasmi wa maji wa shirika hilo.

Meneja wa DAWASCO Mkoa wa Ilala, Christian Kaoneka akiongea na waandishi wa habari juu Mpango huo.

Hivyo limewataka wamiliki hao ambao awali wengi walikuwa wakiiba maji ya DAWASCO na kuyaelekeza kwenye visima vyao kuacha mara moja tabia hiyo, ambayo iko kinyume cha sheria.

Limesema limeamua kufanya hivyo kuwaepusha wakazi wa Dar es Salaam, dhidi ya matatizo yanayoweza kuwapata kwa kushirikiana na wahujumu wa shirika, ambao idadi yao kubwa wanamiliki visima hivyo kwenye maeneo yao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Meneja wa DAWASCO mkoa wa huduma wa Ilala, Christian Kaoneka, ambaye alitoa wito kwa walio nje ya mtandao wa shirika hilo, kujitokeza ili waunganishwe kwenye huduma hiyo.

Akielezea juu ya mpango huo, Kaoneka alisema kipindi cha nyuma kiasi cha maji kilichokuwa kinazalishwa Ruvu juu na Chini hakikuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wote hususan wa Ilala.

Meneja huyo alisema hali hiyo ilisababisha wakazi wengi kuchimba visima vya maji binafsi ili kupata bidhaa hiyo muhimu kwa uhai wa binadamu.

"Tulikuwa na changamoto ya utoshelezaji wa Maji kwa maeneo mengi ya mji. Uzalishaji maji haukuwa mkubwa hivyo kwa wananchi wengi iliwalazimu kuchimba visima vyao binafsi ili wapate huduma hiyo," alisema.

Aidha aliongeza, "Kwa sasa uzalishaji wa Maji umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka kiasi lita za ujazo milioni 182 hadi lita za ujazo milioni 270 kwa siku.

"Kwa ujazo huu tunaweza kusema kuwa maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam yana utoshelezi mwingi wa maji hivyo tutoe rai kwa wamiliki wote wa visima katikati ya mji kuja ofisi za DAWASCO ili kujiunga rasmi na mtandao wa Majisafi."

Meneja huyo alisema sababu kuu ya kuhamasisha mpango huo ni baada ya kugundua wamiliki wengi wa visima hufanya maunganisho ya maji ya DAWASCO bila kufuata taratibu husika na mwisho hudai maji wanayotumia ni ya kisima.

Alisema utamaduni huo umekuwa chanhamoto kwao kwa sababu wakati mmiliki akidai maji yake ni ya kisima, wao huyapima na kubaini ni maji ya DAWASCO ambayo yameelekezwa kuingia ndani ya kisima hiko.

Pamoja na hilo, aliyataja maeneo ya manispaa ya Ilala ambayo yana idadi kubwa ya visima kwa watu binafsi kuwa ni Kariakoo, Upanga na katikati ya jiji.

Habari Kubwa