Wanaoshinda na "Earphone" masikioni muda mrefu waonywa

03Mar 2019
Beatrice Shayo
Dar es salaam
Nipashe Jumapili
Wanaoshinda na "Earphone" masikioni muda mrefu waonywa

SERIKALI imesema wanaoshinda na spika kwenye masikio (Hearphone) kwa muda mrefu wapo hatarini kupata matatizo ya usikivu na kuwataka kuacha mara moja ili wasije kupata huo ugonjwa.

Hayo yalisemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu siku ya usikivu duniani iliyofanyika katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Mloganzila. Alisema wanachi wanatakiwa kupunguza tabia ya kuweka Spika masikioni kwa muda mrefu ili waweze kujikinga na tatizo la ukosefu wa usikivu. " Utakuta kijana akiamka yupo na "Earphone" masikioni muda wote tupunguze hii tabia tusipokuwa makini tunaweza kuwa na taifa lisilosikia kwa sababu ya matumizi ya simu za kisasa pamoja na kuweka spika kwa muda mrefu masikioni,"alisema Aidha, Mwalimu alisema atawasiliana na Shirika la Viwango nchini (TBS) kuhakikisha spika zinazoingizwa Tanzania zinakuwa na ubora unaotakiwa kwa kuwa amepatiwa taarifa bidhaa hiyo kuwepo na feki jambo ambalo litaenda kuongeza tatizo ya usikivu. " Mtoto hadi wa miaka mitatu anawekewa Airphone masikioni sio vizuri tuwe makini katika hilo kwani inachangia ukosefu wa usikivu, hivyo tuchukue tahadhari," alisema waziri. Waziri Mwalimu alisema inakadiriwa zaidi ya asilimia tano ya watu dunia ambao ni sawa na milioni 466 wana ukosefu wa usikivu . Miongoni mwa watu hao milioni 432 ni watu wazima na milioni 34 ni watoto. Alisema ifikapo mwaka 2050 zaidi ya watu milioni 900 watakuwa na ukosefu wa usikivu. Alisema katika hospitali ya MNH wagonjwa waliohudumiwa katika idara ya masikio, pua na koo kati ya Novemba 2018 na Januari 2019 ni 5,959 na kati yao wagonjwa 454 sawa na asilimia nane walikuwa na ukosefu wa usikivu. Aidha, alisema katika kukabiliana na tatizo hilo serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo tiba kwa wagonjwa wenye ukosefu wa usikivu . Alisema mwaka 2018 wagonjwa 117 walipatiwa vifaa vya kukuza mawimbi ya sauti na 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio. Mwalimu alisema kwa mwaka huu kipaumbele chao ni kuboresha huduma za usikivu katika hospitali za rufaa kwa kuwa bado zinachangamoto.

Habari Kubwa