Wanaotaka kufanya mitihani ya bodi sasa kuomba mtandaoni

17Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaotaka kufanya mitihani ya bodi sasa kuomba mtandaoni

MATUMIZI ya mfumo wa usajili wa kupitia kwenye mtandao umezinduliwa rasmi leo jijini Dar es salaam ili kuwezesha watahiniwa wanaoomba  kufanya mitihani ya bodi wautumie badala ya kwenda kwenye ofisi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya wataalam wa ununuzi na ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya wataalam wa ununuzi na ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi ameyasema hayo leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wakati wa maonyesho ya vyuo vikuu  yanayoendelea uwanjani hapo.

Mbanji amesema wanafunzi hao kuanzia sasa wanaweza kutumia simu zao za mikononi kufungua na kuomba kufanya mitihani mtandaoni.

"Kwa wale wote wanaoomba usajili wa kitaalam wanaweza kufanya hatua mbalimbali za usajili wakiwa majumbani kwao na ofisini kwao. Mwanzoni tulikuwa na usumbufu kidogo mtu alikuwa anatoka mkoani hadi ofisini kwetu, kwa sasa hiyo imekwisha," amesema.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB)  Godfred Mbanyi akizungumza na waandishi wa habari leo wakati wa maonyesho ya vyuo vikuu jijini Dar es Salaam.

Pia amesema katika bodi yao huwa wanaendesha matukio mbalimbali, kama kutoa mafunzo ya muda mfupi, mafunzo mahususi katika taasisi.

"Ulipiaji wa huduma hizo  ufanyike mtandaoni kwa sababu katika mfumo ambao tuna uzindua leo ukiingia utakuelekeza hatua kwa hatua na namna ya malipo yatakavyofanyika badala ya kwenda benki kupanga foleni," alisema.

Amesema mfumo huo ni shirikishi wameuboresha kwa kushirikiana na serikali mtandao, umefuata vigezo na taratibu zote za kiserikali," amesema.