Wanaotaka kuhama Ngorongoro wataka mchakato uharakishwe

03Apr 2022
Godfrey Mushi
NGORONGORO
Nipashe Jumapili
Wanaotaka kuhama Ngorongoro wataka mchakato uharakishwe
  • Serikali izuie asasi za kiraia zinazoingilia mchakato

WAWAKILISHI wa wananchi walioamua kuhama kwa hiari kutoka Kata 10, kati ya 11 zilizopo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa kuwaondoa eneo hilo kabla ya kipindi cha kiangazi kufika.

Aidha, wananchi walio tayari kuhama, wameomba vyombo vya dola kuongeza ulinzi kwa wananchi walioonyesha nia ya kuhama, kwa kuwa baadhi ya viongozi wa mila wa jamii ya kifugaji ya Kimasai na viongozi wengine wa kisiasa na vijiji wanawatisha.

Waliotoa ombi hilo Leo ni wawakilishi kutoka Kata za Enduleni, Kakesio, Aleilai, Alaitole, Nainokanoka, Olbalbal, Misigyo, Engaresero, Olorieni na Kata ya Ngorongoro.

Akizungumzia uhitaji huo, mwakilishi wa wananchi wa Kata ya Endulen, Foibe Lukumay,  alisema wananchi hao, hasa wa jamii ya kifugaji ya Kimasai wanatamani kuondoka Ngorongoro na kwenda kwenye makazi mapya ili wakaanze shughuli za kiuchumi kwa uhuru na upana zaidi.

“Nimeamua kuhama kwa hiari yangu, japokuwa napata vitisho katika eneo ambalo ninaishi hasa kutoka kwa viongozi, ndio maana wengi hawataki kuhama.

‘Hata sasa, mimi nimepata vitisho kama Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, kama Makamu Mwenyekiti Baraza la Wazee wa CCM wa Wilaya ya Ngorongoro, lakini nikaamua kwa hayo yote niondoke kwa hiari ili tuweze kuinusuru Ngorongoro. Wanyamapori waweze kuwapo maana wameongezeka kwa kweli. Wameongezeka maana mpaka hata kwangu, wanalala mpaka hapo nje.”

Mwakilishi mwingine wa Kata ya Olbalbal, Christopher Oloju, alisema ameona ni vyema aondoke eneo hilo ili kuitikia wito wa serikali kama ilivyoelekeza.

 “Nimekubaliana na baadhi ya familia  yangu, ila suala la kufika kule na kuona eneo ni jambo zuri. Nikifika pale (Msomera), hata ile familia yangu nitawahamasisha kuhama. Mahali popote unapoenda ni vyema uelewe kwanza unapokwenda, ukaona kwa macho na kujiridhisha na kuona maendeleo yanayoelezwa.

“Pia naomba nisisitize elimu sana itolewe, kwa kuwa elimu ikitolewa vizuri basi mtu anaweza akawa na ule uhiari.

Saning’o Laizer, Mkazi wa Kijiji cha Endeleni, alisema "Kuna watu wengine sasa, hata watu wamekuwa tayari kuitikia wito huo wanatishwatishwa, wanadanganywadanganywa.

"Wengi wanasita kuhama kwa sababu elimu ni ndogo kwa wengi wetu. Mimi nimejiandikisha kwa Mkuu wa Mkoa.

"Mimi nimeenda Msomera, nimeona nyumba zinazojengwa ambazo tutakaa kwa kweli huku kuzipata ni ndoto, nimekaa pale siku mbili. Nimeona nyumba nzuri vyumba vitatu na sebule, aekari tatu zinazozunguka hiyo nyumba pamoja na ekari tano za kulima na kufuga na, nimeambiwa unapewa hatimiliki ambayo huku Ngorongoro ni ndoto."

Kuhusu baadhi ya Asasi za kiraia au Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), kudaiwa kufadhili fedha na kuhamasisha wananchi wasihame ili kuharibu mchakato wa kuhama kwa hiari, Mwakilishi wa wananchi hao Paulo Mamasita, Mkazi wa Kata ya Ngorongoro alisema: “Hili suala la kuhama watu wako tayari kuhama lakini kuna vitu na watu wanaangalia upepo. Lakini mbali na kuangalia upepo kuna mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoendeshwa na watu binafsi wanaingilia mchakato huu. Wanafanya kampeni za hapa na pale kuwashawishi wale ambao wako tayari wasiondoke.

“Na sijaelewa kwa nini lakini kwa uelewa wangu ama ninavyoona mimi pia wanafaidika kupitia michakato hiyo. Ile kwenda kushawishi wao wanapata fedha kwa donors (wafadhili), hawajui wanamuumiza yule mtu wa hali ya chini, kwa sababu yule hajasoma hawezi kuona vitu kwa mapana zaidi kama yeye.

“Wanatumia hilo kama kitega uchumi maana unakuta hao wote wanaoeneza haya mambo maisha yao yako vizuri mjini, wana kazi, watoto wanasoma mjini international school (shule za kimataifa), lakini tukija kwenye uhalisia hawa watu wa chini waliopo kwenye jamii hawajasoma wao.

“ Wanasumbuliwa sana hivyo wanashindwa kutoa maamuzi ambayo ni sahihi. Kwa hiyo serikali iyaangalie mashirika baadhi ya watu binafsi, japokuwa wanajulikana. Wazuiwe kuingilia mchakato kama huu kwa sababu kuingilia mchakato huu ni kuingilia mawazo ya mtu na uhuru wa mtu binafsi.”

Aidha, Mamasita alisisitiza kuwa kuhama kwa hiari ni jambo la mtu binafsi na ni suala la mtu mwenyewe kuona kwamba lina faida ama halina faida. Akitaka asitokee mtu kwa namna yeyote akaingilia uhuru wa mtu mwingine.

“Suala la kuhama kila mtu analiangalia kama lina fursa ama halina fursa.Mimi na mke wangu tuliona ni suala la muhimu sana na ni vizuri tuiunge mkono serikali ili kupisha suala la uhifadhi.

“Tumeona kwamba kuna migogoro sana ndani ya hifadhi kulingana na kwamba lile ni eneo la serikali na ni eneo la hifadhi watu wanaongezeka, kila leo wanyama wanazaliana, mifugo inazaliana lakini caring capacity (uwezo wa kuchukua) lile eneo ambalo lina idadi kubwa ya mifugo, watu na wanyama halibadiliki liko palepale.”

Vilevile, alishauri kwenye makazi mapya ambayo serikali imeandaa, anaomba serikali iangalie na iweke miundo mbinu yote, ambayo ni muhimu kwa maisha ya binadamu.

“Nikisema miundombinu ni pamoja na shule, walimu wawepo. Jingine ni suala la afya, zahanati iwe imeshaandaliwa pale na wataalam wote wa afya hasa madaktari, wauguzi wawepo pale, kwa sababu kama tunavyojua suala la afya ni jambo muhimu sana,”alieleza Mamasita

Mwakilishi wa Kata ya Nainokanoka, Emmanuel Saitoti, alisema kuwa vijana wengi wa Ngorongoro wamekwenda Kenya kulinda na maeneo mengine, kwa ajili ya kujitafutia riziki kutokana na kuona maisha ya Ngorongoro ni magumu. 

 

Alisema vijana wana fursa nyingi wanazipata wakiwa nje ya Ngorongoro, lakini wakiwa ndani hawawezi hata kuendesha bodaboda. Vijana wengi wanapigwa na kufa huko walipo nchi jirani

 

Kisumu sababu fursa Ngorongoro haziruhusu kujikwamua kichumi hivyo ni sahihi kuondoka Ngorongoro kwasababu hawapati huduma muhimu kwa jamii

 

Alisisitiza pia lishe kwa watoto wadogo ni changamoto hivyo ni wakati wa kuungana kwa pamoja ili wajikwamue kiuchumi kwani lishe ni duni na hata fursa za kujikwamua kichumi nazo ni hafifu kwa vijana.

 

Naye, Ngeresai Ndaskoi, Mkazi wa Oldimbau, Kata ya Misigyo alisema: “Nikionyeshwa kwamba hapa kuna Dispensary (Zahanati), Shule ya Msingi na Sekondari watoto wangu watasoma. Nataka niwe na mahali pa kuishi, nataka niwe na shamba la kulima na mahali mifugo yangu itaishi, kwa sababu nategemea mifugo.

“Huu udongo, ardhi ndio mafuta yetu, kila kitu nikiona kwamba hapa kuko vizuri naweza nikakubali.Naomba niende nikaone mahali napokwenda ni wapi.”

Habari Kubwa