Wanaotelekezewa familia watakiwa kutoa taarifa

25Feb 2020
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Wanaotelekezewa familia watakiwa kutoa taarifa

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani jamii mkoani Katavi imetakiwa kutoa taarifa sehemu husika pale inapoona kuna mtu anafanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kutelekezewa familia.

Mkuu wa mkoa wa katavi, JUMA HOMERA akizungumza na watumishi pamoja na wananchi kuhusu ukatili wa kijinsia.

Akizungumza katika ufunguzi wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambayo imeziduliwa leo Februari 25,2020 Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuna wanaume wanafanyiwa ukatili lakini wanaogopa kusema kwa kuhofia kuchekwa.  

Homera alisema kuna kesi nyingi ambazo zinawafikia  wao kama viongozi za masuala ya ukatili huku nyingi zikiwa ni wanaume kutelekeza watoto na kumuachia mzigo mwanamke.

"Kuna familia nyingi sana humu zimelelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama na kuna wengine nawafahamu wanalea watoto wao wenyewe baba zao wakiwa wamewakimbia kesi nyingi sana za namna hii zinatufikia huu nao ni ukatili hata mimi nikizalisha alafu nikamkimbia mtoto inabidi nikamatwe niwekwe ndani,"alisema Homera.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii, Imelda Evelyne Kamuguisha akizungumza na wananchi kuhusu ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii, Imelda Kamugisha, ambaye ni kiongozi wa msafara wa kijinsia unaolenga kutokomeza vitendo vya kikatili kuelelekea Siku ya Wanawake Duniani alisema msafara umeamua kuanza na Mkoa wa Katavi kutokana na takwimu kuonyesha kuna ndoa nyingi na mimba za utotoni.

"Kwanini tumeamua kuanza na Katavi na sio mkoa mwingine ni kwa sababu takwimu zinaonyesha mkoa huu una ndoa nyingi na mimba za utotoni na ukatili mwingine ambao umeongezaka aliousema mkuu wa mkoa ukatili wa utelekezaji,"alisema kamgisha.

Alisema tafiti za afya zinaonyesha umri kati ya miaka (15-49) ambayo ni asilimia 40 ya wanawake wamefanyiwa ukatili na watoto Kati ya umri wa miaka (15-19) ambayo ni asilimia 27 wamezaa katika umri mdogo.

Msafara huo wenye lengo la kupinga ukatili wa kijinsia wenye kauli mbiu isemayo " tokomeza ukatili wa kijinsia twende pamoja" unatarajiwa kufikia mikoa 9 ambayo ni Katavi,Rukwa,Songwe,Mbeya, Njombe,Iringa, Tabora, Shinyanga,na Simiyu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera akiagana na Msanii Shetta mara baada ya kuzindua Msafara wa kijinsia wa kutokomeza ukatili leo mkoani Katavi.

Habari Kubwa