Wanaotumia corona kujitafutia kiki ya kisiasa waonywa

15Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Wanaotumia corona kujitafutia kiki ya kisiasa waonywa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaasa wanasiasa nchini kutotumia mlipuko wa virusi vya corona uliotokea nchini China kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, aliwataka Watanzania waendelee kuitegemea serikali katika kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala mbalimbali zikiwamo na za mlipuko wa virusi hivyo na kusisitiza “tusiupotoshe umma.”

Aliyasema hayo jana baada ya kushiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuliombea taifa ili kuliepusha na maafa mbalimbali.

Alisema katika mji wa Wuhan ambako virusi hivyo vilianzia, wapo Watanzania 497 na kwamba wote wapo salama na serikali inaendelea kuwasiliana nao kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na ubalozi.

“Taifa hili ni muhimu sana kwetu na ni msingi wa maisha yetu, hivyo watu wasiwe wanapotosha umma na kuwatia hofu Watanzania, vijana wetu wapo salama. Pia tumejipanga kukabiliana na majanga hayo ikiwa ni pamoja na nzige. Tumuombe sana Mwenyezi Mungu atuepushe”

Wakati huohuo, ugonjwa wa corona umezidi kuongeza hofu duniani baada ya watu 59,804 walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo nchini China.

Taarifa ya Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam ilisema wagonjwa hao ni wa China Bara na kwamba kati yao 5,911 walipona na kuruhusiwa kutoka hospitalini wakati 1,367 walikufa na 52,526 wanaendelea kupata matibabu.

Ilisema hadi Februari 12 kulikuwa na wagonjwa 13,435 walioshukiwa kuambukizwa waliokuwa wakisubiri kupata majibu ya vipimo wanaotoka maeneo ya China Bara.

Aidha, ilisema huko visiwani Hong Kong, Macao na Taiwan, watu 50 walithibitishwa kupata ugonjwa huo wakati 10 waliripotiwa Macao na Taiwan walikuwa 18, hapo Februari 12.

Iliongeza kuwa wiki hii Februari 12, Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC ilikutana kwa mara ya tatu kujadili hali ya kuzuia na kudhibiti homa ya corona -COVID-19. Ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC na Rais Xi Jinping.

Ilisema mkutano huo ulitaka kutatua fumbo la kudhibiti janga kwa kuinua viwango vya kulaza wagonjwa hospitali na viwango vya tiba na kupunguza maambukizi na viwango vya vifo.

Taarifa ilisema aidha, ilitoa wito wa juhudi za kuboresha matibabu kwa wagonjwa, hasa walio katika hali mbaya, kwa kutumia rasilimali bora zaidi za kitabibu na kiteknolojia, kufanya mapitio ya wakati mwafaka ya suluhiho la utambuzi na matibabu na kuongeza maendeleo ya dawa na chanjo.

Rais Xi Jinping, aliagiza wafanyakazi wa matibabu zaidi ya 2,600 kusaidia vita dhidi ya mlipuko wa COVID-19 huko Wuhan na ujumbe wa matibabu wa PLA unashughulikia hospitali mbili katika mji huo na utafanya kazi chini ya Hospitali ya Huoshenshan, ambayo ni ya kwanza ya muda iliyoanzishwa mapema Februari wakati wa janga hilo.

Ilisema kufikia Februari 13, Jeshi la Ukombozi la Watu wa China -PLA limepeleka vikundi vitatu vya wafanyakazi zaidi ya 4,000 wa matibabu Wuhan tangu kuzuka kwa janga hilo.

Habari Kubwa