Wanaouza maji kwa magari waitwa kujisajili, zimebaki siku sita

24May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Wanaouza maji kwa magari waitwa kujisajili, zimebaki siku sita

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) imewataka wamiliki na madereva wa magari ya kuuza maji safi (Water Bowsers) jijini Dar es salaam na Pwani kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kusajiliwa na kupewa kibali kabla zoezi hilo halijafungwa Mei 29 mwaka huu.

magari ya kuuza maji yakiwa katika foleni ya kupakia maji tayari kwa kwenda kuuza kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Afisa kutoka kitengo cha Mawasiliano kwa umma DAWASA, Joseph Mkonyi, amesema zoezi hilo linakwenda vizuri ambapo amewataka wamiliki ama madereva kutumia siku zilizobaki kukamilisha usajili ili waweze kupewa kibali cha kuuza majisafi kwa wananchi.

"Niwaombe watu wote ambao wanafanyabiashara ya kuuza maji safi kwa kutumia magari (Water Bowsers) wajitokeze ili tuweze kuwatambua tuwasajili na kuwapa leseni sambamba na kuwapa mikakati yenye lengo la kujenga ili watoe huduma bora..Zimebaki siku sita zoezi hili kuhitimishwa zoezi hili, tunawaomba wamiliki wa magari kuona umuhimu wa jambo hili ili kuepuka usumbufu hapo baadae." Amesema Mkonyi

Mkonyi ameongeza lengo la zoezi hilo ni kuhakikisha kuwa wateja (wananchi) wanaopata maji kupitia magari hayo wanapata huduma bora kutoka vyanzo rasmi vya maji vinavyotambuliwa na DAWASA.

Amesema kuwa baada ya muda wa usajili kuisha, gari yoyote ya Majisafi itakayokutwa katika eneo la huduma la DAWASA ikitoa huduma bila leseni ya uendeshaji, itachukuliwa hatua kali za kisheria . Wananchi wanashauriwa kutumia Magari ya kusambaza Majisafi yaliyosajiliwa na DAWASA.

Vitu muhimu kwa ajili ya usajili

1. Picha moja ya rangi ya mmiliki wa gari na nakala ya kitambulisho chake (KURA, UTAIFA AU HATI YA KUSAFIRIA)

2. Nakala ya kadi ya gari, nakala ya bima ya gari na nakala ya leseni ya dereva  (vithibitishwe na Mwanasheria)

Pia matenki ya Magari yatakayokidhi vigezo vya kupata usajili yatasafishwa na yatawekewa  dawa maalumu ya kuua wadudu kwenye matanki ya gari  na kubandikwa stika za DAWASA.

Usajili na utoaji leseni za uendeshaji litafanyika katika eneo la Chuo Kikuu Ardhi kwenye matanki ya DAWASA Maarufu kama (Terminal). Gharama ya usajili ni Tsh 100,000/= (itakayolipwa baada ya kukamilisha vigezo vyote.

Afisa kutoka kitengo cha Mawasiliano kwa Umma DAWASA, Joseph Mkonyi (kulia) akitoa maelekezo ya cheti kwa dereva mara baada ya kumaliza zoezi la ubandikaji wa stika ya utambuzi itakayomuwezesha kuendelea kutoa huduma ya kuuza majisafi jijini Dar es Salaam. 

Habari Kubwa