Wanataaluma ARU wapigia debe umuhimu wa mipango miji

04Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanataaluma ARU wapigia debe umuhimu wa mipango miji

WANATAALUMA wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU) wameishauri serikali kulipa kipaumbele suala la mipango miji kwa kuhakikisha maeneo mengi yanapimwa na kuwekewa huduma muhimu ili wananchi wanapofika wasijenge holela.

Ushauri huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa kongamano la tisa la wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Haruna Masebu, wakati wakijadili masuala ya mipango miji, ardhi na makazi nafuu.

Mada kuu kwenye kongamano hilo la wanataaluma wahitimu wa chuo hicho ilikuwa kuelekea kwenye kupatikana kwa ardhi na makazi nafuu kwenye kaya zenye kipato cha chini nchini miaka 60 baada ya Uhuru.

Masebu alisema waliamua kuzungumzia masuala ya makazi nafuu kuangalia namna nchi ambavyo imesaidia wananchi wake tangu uhuru kupata makazi nafuu kwa kuwa makazi ni jambo la msingi kwa binadamu.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo la wanataaluma wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), akichangia mada wakati wa kongamano hilo lililofanyika chuoni hapo siku ya Ijumaa ambapo mada kuu ilikuwa kuelekea kwenye kupatikana ardhi na makazi nafuu kwa kaya zenye kipato cha chini miaka 60 baada ya Uhuru.

“Tumeona ni vizuri kuangalia tulipotoka tulipo na tunapoelekea kwenye suala la makazi ila tumeona changamoto kubwa ya watu kuishi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa wanaishi sehemu hazijapangwa hivyo wanakosa huduma muhimu,” alisema

Alisema kuna umuhimu kwa serikali kuweka mipango kuhakikisha wananchi wanaishi na kujenga kwenye maeneo yaliyopangwa kwa kuweka miundombinu na mahitaji yote muhimu.

Alisema bado kuna changamoto ya kupata fedha za kujenga makazi hivyo wanatumia muda mrefu kujenga nyumba hivyo wasomi wamejadili namna ya kuwezesha wananchi kujenga kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.

Washiriki wa Kongamano la wanataaluma wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo lililofanyika chuoni hapo jana jijini Dar es Salaam.

Alisema miongoni mwa majukumu yanayowakabili wanakongamano hao ili kujenga  taasisi imara yenye heshima ni kuhakikisha hosteli za chuo hicho zinakuwa na taa za barabarani na kujenga jingo kubwa litakalokuwa na shughuli mbalimbali.

“Kongamano hili linapaswa kushirikiana na ARU na washirika wengine katika kutimiza majukumu yake na mafanikio yetu mengi yatategemea namna tunavyoshirikiiana na wengine hivyo natoa wito kwa baraza la wahitimu kufanyakazi kwa bidii, kuweka mikakati kabambe na kuwa na maono ya muda mrefu kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa haraka na kwa wakati,” alisema

Washiriki wa kongamano la wanataaluma waliowahi kusoma  Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wakifuatilia kwa karibu mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kongamano lililofanyika chuoni hapo siku ya Ijumaa. Kushoto kabisa ni Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Haruna Masebu.

Habari Kubwa