"Wanaume wa Mbeya wanapenda kulelewa" - Chalamila

21Nov 2020
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
"Wanaume wa Mbeya wanapenda kulelewa" - Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema asilimia kubwa ya Wanawake wa mkoa huo wanaongoza kubeba jukumu la kuendesha familia zao kuliko wanaume.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Chalamila ameyasema hayo leo Novemba 21,2020 wakati akifunga Kongamano la sita  la Jinsia ngazi ya wilaya ambalo linafanyika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Amesema wanawake wengi mkoani humo ndio wamebeba jukumu la kutunza na kulea familia  na hufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali ikiwemo kuuza mboga mboga na matunda wakati wanaume wakitumia mwanya huo kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni  pamoja na kuny'ang'anya fedha wanazopata kwenye biashara na kwenda kuhonga michepuko.

Amesema moja ya mambo yanayochangia masuala hayo ni baadhi ya wanaume kuendekeza mfumo dume katika suala la umiliki wa ardhi na uchumi.

" Idadi kubwa ya wanaume mkoani Mbeya wanapenda kulelewa hawapendi kujishughulisha wanawategemea wanawake kulisha familia na kufanya kila kitu, mbaya zaidi huwashinikiza wake zao kuomba mkopo kwa kutumia akaunti zao ili wazulumu hizo hela, nawaambia wanawake msikubali kutumika kama ndoa yako ina shida  ondoka kaanzishe maisha mengine," amesema Chalamila

Habari Kubwa