Wanaume Shinyanga walalamika kunyimwa unyumba na wake zao

07Dec 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Wanaume Shinyanga walalamika kunyimwa unyumba na wake zao

BAADHI ya wanaume mkoani Shinyanga, wamelalamika kufanyiwa vitendo vya  ukatili wa kijinsia na wake zao kwa kunyimwa unyumba.

Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga Brihgtone Rutajama, akitoa elimu ya ukatili wa kinjisia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo.

 

Wamebainisha hayo leo wakati dawati la jinsia la Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga, lilipokuwa likitoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo.

Mmoja wa wanaume hao Peter Makalanga, amesema wanawake wamekuwa wakiwafanyia ukatili mkubwa waume zao, kwa kuwanyima unyumba hata ndani ya wiki mbili, kwa madai ya kuchoka na kazi.

"Tunashukuru kwa elimu hii ya ukatili wa kijinsia kutuletea hapa Stendi, lakini wanaume tuna nyanyasika sana siku hizi, wake zetu wanatunyima unyumba, lakini akijua unachepuka ndipo mgogoro unapoanzia na kufikia hatua ya kupigana," amesema Makalanga.

Mwanaume Peter Makalanga, akilalamika vitendo vya ukatili ambavyo hufanyiwa wanaume na wake zao kwa kunyimwa unyumba.

"Waambieni na wake zetu wasitufanyie ukatili, lakini wao ukiwagusa tu tayari wanakimbilia Polisi kushitaki, hiyo siyo sawa, lakini ukiangalia chanzo cha yote hayo ni yeye mweyewe kuni nyima unyumba," ameongeza. 

Aidha, amesema na migogoro inapotokea ndani ya familia, ndiyo chanzo cha kuachana na kusababisha watoto kukosa malezi bora, na hata kuwa machokolaa mitaani na wakike kujiuza.

Kwa upande wake Mkuu  wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga, Brightone Rutajama, amewataka wanaume kufika kwenye dawati hilo kutoa taarifa za kufanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao na siyo kuona aibu.

Amesema kwenye dawati hilo la jinsia, wanapokea malalamiko ya watu wote bila ya ubaguzi, na kisha kuyatafutia ufumbuzi ikiwamo kutatua migogoro ya ndoa, lakini wanaotoa taarifa za kufanyiwa ukatili wengi hua ni wanawake.

Katika hatua nyingine, amewataka wafanyabiashara wa Standi ya Mabasi wilayani Shinyanga, Bodaboda, Bajaji na Mawakala, kuacha kufanyiana vitendo vya ukatili wa kijinsia,ikiwamo kutoleana lugha chafu za matusi ya nguoni.

Wafanyabiashara, Mawakala wa Mabasi, Bodaboda na Bajaji, akisikiliza elimu ya ukatili wa kijinsia kutoka Dawati la Polisi wilayani Shinyanga.

Naye Mratibu wa Polisi Jamii wilayani Shinyanga, Magesa Marwa, akizungumza na Madereva wa Bajaji pamoja na Bodaboda kwenye Standi hiyo, amewataka kuwa mabalozi wazuri katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia amewataka madereva hao wa Bajaji na Bodaboda, katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, wazingatie sheria za usalama barabara, ili kutosababisha ajali ambazo ugharimu maisha ya watu na wengine kupata ulemavu.

Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga Brihgtone Rutajama, akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo.