Wanaume vinara vifo vya UKIMWI

20May 2022
Sanula Athanas
MOROGORO
Nipashe
Wanaume vinara vifo vya UKIMWI

WATU 54,000 nchini wamepata maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini kwa mwaka 2021 huku ripoti mpya ikibainisha kupungua kwa maambukizi hayo kulinganishwa na mwaka 2020 ambao watu 68,000 walipata maambukizi mapya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko.

Hayo yalibainishwa jana mjini Morogoro na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, aliporejeshwa ripoti mpya ya zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi HIV/AIDS (UNAIDS).

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa wahariri na waandishi wa habari, Dk. Maboko alisema ripoti mpya inaonyesha juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau kukabiliana na VVU/UKIMWI zimekuwa na matokeo chanya.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema bado kunahitajika nguvu zaidi ili kuzuia maambukizo mapya ili kupunguza kasi ya maambukizo.

 

Dk. Maboko alibainisha kuwa vifo vitokanavyo na UKIMWI nchini vimepungua hadi 29,000 mwaka 2021 kutoka vifo 32,000 mwaka uliotangulia, yaani 2020.

 

"Ukiangalia takwimu za vifo, wanaume wanaoongoza wakati wanawake wanaoongoza kwa maambukizi. Hii ina maana kwamba wanaume wako nyuma kujitokeza kupima na wako nyuma kutumia ARVs (dawa za kupunguza makali ya VVU).

 

"Wanawake ni wepesi kupima na wanatumia vizuri dawa. Tunamshukuru Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) amekubali kuwa balozi wa wanaume kuhamasisha upimaji kujua hali ya maambukizi ya VVU," alisema.

 

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alipotakiwa kuweka wazi takwimu za uwiano halisi wa vifo vya wanaume na wanawake vitokanavyo na UKIMWI, alisita kwa ufafanuzi kwamba: "Ripoti kamili itatangazwa baadaye".

 

Alisema malengo ya Tanzania ya 95-95-95, kwa maana ya asilimia 95 yapime kujua hali zao kiafya, asilimia 95 wanaobainika kuambukizwa waanze kutumia dawa na asilimia 95 wawe wamepunguza makali ya virusi, yanatekelezwa vizuri ili kulifikia lengo kuu la kudhibiti janga 'HIV/AIDS Epidemic Control' kufikia mwaka 2030, ambao ni ukomo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Dk. Maboko alisema makadirio mapya yanaonyesha vijana wanaendelea kuwa kundi lililo hatarini zaidi dhidi ya VVU/UKIMWI, hivyo programu nyingi sasa zimeelekezwa kwa kundi hilo.

 

Alisema ili kudhibiti kuenea kwa virusi, watu wote wanapaswa kupima kujua hali ya maambukizi na wanaobainika kuwa na maambukizi waanze kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU.

 

"Kama watu hawajui hali zao kuhusu VVU, hawawezi kujikinga wao wenyewe, familia zao, wenzao wao. Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yalianza miaka mingi iliyopita lakini hayajafanikiwa kufikia lengo kutokana na vikwazo mbalimbali, ukiwamo unyanyapaa, mtazamo hasi dhidi ya VVU/UKIMWI, kutokuwa na elimu kuhusu suala hilo na kutotumia dawa," alifafanua.

 

 

HALI ILIVYO

 

Nyangusi Laiser, Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini TACAIDS, akirejea takwimu za kitaifa na kimataifa, alibainisha kuwa kwa mwaka 2020, kulikuwa na watu milioni 37.7 waliokuwa wanaishi na VVU duniani.

 

Kati yao, watoto wenye umri chini ya miaka 15 ni milioni 1.7 na kwamba asilimia 53 ya waliokuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi walikuwa wanawake.  Alisema maambukizi mapya kwa mwaka 2020 yalikuwa watu milioni 1.5, kukionekana kuwapo kupungua kutoka watu milioni tatu mwaka 1997.

 

"Takwimu zinaonyesha kila siku takriban watu 4,000 huambukizwa VVU duniani na kati yao, 2,400 (asilimia 60) ni waliopo kusini mwa Jangwa la Sahara," alibainisha.

 

Kwa Tanzania, ofisa huyo alisema kuwa kwa mwaka 2020, watu waliokuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi walikuwa milioni 1.6. Kati yao, wanawake ni milioni moja na wanaume 600,000.

 

"Maambukizi mapya mwaka 2020 nchini yalikuwa watu 58,000. Kati yao, 37,000 ni wanawake, wanaume 21,000 na ndani ya makundi hayo kuna watoto wenye umri chini ya miaka 15 wapatao 10,000. Vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 wanaongoza kwa maambukizi mapya wakiwa asilimia 80 kwenye idadi hiyo ya watu 58,000 waliopata maambukizi mapya.

 

"Mikoa yenye maambukizi makubwa inaongozwa na Njombe asilimia 11.4 na Iringa asilimia 11.3. Pia mikoa ambayo watu wake wako nyuma katika kupata huduma za tohara imeonekana kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi," alifafanua.

 

Alizitaja njia kuu za maambukizi kuwa ni ngono asilimia 80, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto asilimia 18 na maambukizi kwa njia ya kitabibu asilimia 1.8.

 

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya DARE, Dk. Lillian Benjamin, akiwasilisha mada kuhusu uelewa wa VVU/UKIMWI, alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kupima, akisisitiza kuwa anayeanza kutumia dawa mapema, anakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutopata madhara makubwa na hata kuepuka kuambukiza wengine.

Habari Kubwa