Wanaume wakiri kuuza mazao kununua ngono

12Dec 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanaume wakiri kuuza mazao kununua ngono

BAADHI ya wanaume wa kijiji cha Butini Kata ya Itwangi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamekiri kuuza mazao ili kununua ngono kutoka kwa wanawake (Makahaba), ambao hutoka mijini kwenye kipindi cha mavuno na kwenda vijijini kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono ili kuchuma fedha za mavuno-

Peter Shilinde aliyekiri kuwa ni miongoni mwa wanaume waliokuwa wanauza mazao na kununua ngono kutoka kwa makahaba.

-kutoka kwa wanaume wa kijiji hicho.

Wamedai kuwa kinapofika kipindi cha mavuno ya mazao hua kuna ongezeko la wanawake wengi weupe kutoka mjini, ambao hufika kijijini humo kwa ajili ya kufanya biashara ya kuuza ngono, ambapo baadhi yao hushawishika na kuamua kuuza mazao na kumpatia fedha mwanamke ambaye amempenda na kushiriki naye ngono.

Mmoja wa wanaume kijijini hapo Peter Shilinde ambaye ana watoto wanne, ametoa ushuhuda kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwa lengo la kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia kijijini humo, ulioandaliwa na Shirika la Kivulini ambalo linatetea haki za wanawake, kuwa yeye ni miongoni mwa wanaume ambao walikuwa wakinunua makahaba kutoka mjini.

Amesema kutokana na makahaba hao kuhitaji fedha nyingi ili wafanye nao mapenzi, kuanzia shilingi 80,000 hadi 100,000, iliwalazimu kuuza mazao yao ya mpunga na kuwapatia fedha hizo ambazo wanazihitaji na kisha kushiriki nao ngono na kama mwanaume hana fedha itabidi ampatie gunia zima la mpunga.

“Kuna tatizo kubwa hapa kijijini kwetu la wanaume kuuza mazao na kwenda kununua ngono kwa makahaba ambao huja vijijini kufanya biashara hiyo kwenye kipindi cha msimu wa mavuno, na mimi nilikuwa ni miongoni mwao lakini nimeshaacha baada ya kuona nazidi kuwa maskini tu,” amesema Shilinde.

“Na wanaume ambao hua wananunua mahakahaba ni wale ambao wanaendekeza masuala ya ulevi, na ukiuza tu mazao unaikimbia familia na kuhamia Sentani kwa muda wa siku mbili au tatu kwenye maeneo ambayo wanaishi makahaba hao, fedha zikiisha unarudi nyumbani kuuza tena mazao mengine”ameongeza.

Teleza Kazilo ambaye ni mhanga wa matukio hayo, amesema mume wake alikuwa na tabia hiyo ya kuuza mazao na kwenda kununua ngono kwa mahakaba wa mjini, na alipokuwa akipinga kitendo hicho alikuwa akiambulia kipigo hadi chakula kinaisha ndani, na kuamua kwenda kufanya vibarua ili watoto wapate chakula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Masanja Ikingo na Mtendaji wa Kata ya Itwangi Claudia Kimaro, kwa nyakati tofauti wamekiri kuwepo na vitendo hivyo na kubainisha lakini wameshindwa namna ya kuwadhibiti makahaba hao ikiwa hua wanakwenda na njia ya kufanya biashara ya kuuza Pombe ama kununua mpunga.

Aidha Ofisa Tathimini na ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini, Godfley Paschal, amesema kijiji hicho cha Butini ni miongoni mwa vijiji vilivyopo kwenye Kata ya Itwangi, ambavyo vinapewa elimu ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo hali ya kiuchumi kwa wanaume kuuza mazao yote na kununua ngono.

Habari Kubwa