Wanaume wanaokimbia familia zao kisa watoto wenye usonji kusakwa

01May 2022
Vitus Audax
MWANZA
Nipashe Jumapili
Wanaume wanaokimbia familia zao kisa watoto wenye usonji kusakwa

Serikali mkoani Mwanza imesema itaanza msako wa kuwabaini wanaume wanaotelekeza familia zao kutokana na kuwa na watoto wenye tatizo la usonji.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya usonji na kulihakikishia  Shirika la Li-TAFO (Living Together Autistic Foundation) linalojihusisha na utambuzi na malezi ya watoto wenye usonji mkoani Mwanza kuwa watawabaini wanaume wanaotelekeza familia zao kisa watoto wenye usonji ili wakazitunze familia zao. Kali, ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, alisema serikali itatoa ushirikiano wakutosha katika suala la kuwasaidia watoto wenye usonji mkoani humo.

"Kumekuwa na tabia ya wanaume kuzitelekeza familia zao kisa watoto wenye usonji niwahase sasa wale  watakao thubutu kuzikimbia familia zao kutokana na watoto wao kuwa na tatizo la usonji, tutawatafuta popote na kuhakikisha wanashiriki malezi ya watoto hao." alisema na kuonfgeza kuwa;

"Tumesikia mnahitaji kiwanja kwaajili ya ujenzi wa kituo cha watoto wenye usonji, sisi kama serikali ya Mkoa wa Mwanza tutawapatia kiwanja ili muweze kukamilisha ujenzi huo" aliongeza.

Akizungumza, katika maadhisho hayo, Daktari wa watu wenye tatizo la usonji Yusufu Jamnangerwalla, aliwataka wanajamii kutokuwaficha ndani watoto hao ili kupunguza ukali wa tatizo hilo.

"Naomba niwaambie wazazi na jamii kwa ujumla, usonji sio ugonjwa, bali ni tatizo ambalo ukiliendekeza linaweza kukua zaidi hivyo niwaombe watoeni watoto wenu wachanyikane na wengine na wataweza kuendana na mazingira" alisema

Habari Kubwa