Wanaushirika tumbaku kujenga kiwanda

23Mar 2019
Halima Ikunji
Uyui
Nipashe
Wanaushirika tumbaku kujenga kiwanda

UMOJA  wa  Vyama  Vikuu   vya Ushirika wa  Tumbaku (TCJE)  umependekeza na kudhamiria kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao hilo mkoani Tabora na kujiwekea lengo la kupata Sh. milioni 700 hadi mwisho wa msimu wa kilimo wa mwaka huu.

Mwenyekiti wa TCJE, Emanuel Charahani, alisema jana kuwa wazo la kiwanda hicho limeshajadiliwa na wajumbe wa vyama vyote kutoka Kigoma, Kahama na Mpanda na kuafikiwa, sasa kilichobaki ni utekelezaji tu.

Alisema wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) kwa kauli mmoja, wameazimia kujengwa kwa kiwanda hicho wilayani Urambo.

Charahani alisema katika kikao hicho, wajumbe hao ambao wote ni wakulima wa zao hilo, walisema kiwanda hicho kitasaidia kuhamasisha kilimo bora cha tumbaku na kuongeza uzalishaji maradufu tofauti na hali ilivyo sasa. 

Mwenyekiti huyo  alisema vyama hivyo  wamedhamiria kujenga kiwanda hicho  ambacho kitaondoa urasimu wa makisio na kuongeza tija katika uzalishaji wa tumbaku na  kutoa zaidi ya ajira  3,000 kila msimu wa kilimo.

Charahani alisema  ili kufanikisha ujenzi huo, alishauri wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri zinazolima  tumbaku, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa na Mrajisi Ushirika wa Mkoa wakutane Aprili 15, mwaka huu katika ofisi za Bodi ya Tumbaku Tanzania ili kuunda kamati ya utekelezaji. 

 Alishauri kuanza mara moja kwa mchakato na upembuzi yakinifu, huku akiutaka uongozi wa WETCU kusimamia ipasavyo mchakato huo ili kuharakisha ujenzi.

Kwa mujibu wa Charahani, hizo ni juhudi za wakulima kuhakikisha wanaungana na wadau kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika maendeleo ya viwanda.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Said Ntahondi, alisema ujenzi wa kiwanda hicho unasubiriwa kwa hamu kubwa na wakulima wa tumbaku nchini kutokana na umuhimu wake.

Alisema wazo la ujenzi wa kiwanda hicho limepata baraka za vyama vyote vikuu vya ushirika wa wakulima wa zao hilo katika mikoa yote na kila mkulima amekubali kuchangia Sh. Tisa kwa kila kilo atakazouza ili kufanikisha ujenzi huo.

Kwa kuchangia kiasi hicho katika msimu huu pekee, alisema wanatarajia  kukusanya zaidi ya Sh. milioni 700 kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba eneo la ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Collins Nyakunga, aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kukaa meza moja na vyama vikuu vya ushirika vya Milambo na WETCU kabla ya kuanza ujenzi huo ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Habari Kubwa