Wanavyuo CUF walia na Polisi Zanzibar

20Dec 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wanavyuo CUF walia na Polisi Zanzibar

UMOJA wa Vijana wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Wananchi (CUF), umelituhumu Jeshi la Polisi Zanzibar kwa madai ya kuwavurugia kongamano lao lililokuwa lifanyike jana visiwani humu.

UMOJA wa Vijana wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Mkurugenzi wa umoja huo, Mohammed Ibrahim Rajab, alisema kongamano hilo lilikuwa lizungumzie mustakabali wa hali ya kisiasa Zanzibar, lakini Jeshi la Polisi liliingilia kati na kuzuia kufanyika.

Mohammed alisema kitendo hicho cha polisi ni cha ukiukwaji wa sheria za nchi na ukandamizaji wa haki za wanafunzi.

Kwa msingi huo, Mohemmed amelitaka jeshi hlo kusimamia misingi ya maadili kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kuheshimu uhuru na haki ya kila raia.

“Kutokana na muktadha wa demokrasia na muendelezo wa matukio mbalimbali nchini, Kamati ya Wanafunzi ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar iliyo chini ya JuviCUF, iliandaa kongamano hilo kwa dhamira ya kujadili mustakbali wa demokrasia na haki za binadamu,” alisema.

Alisema ibara ya 18 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010, inatamka kwamba bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoka nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Hata hivyo, alisema kwa makusudi, Jeshi la Polisi liliamua kuingilia kati na kuvuruga ratiba ya kongamano hilo kwa mbinu, hila na vitimbi.

“ Awali, maofisa hao walitumia mbinu ya kutoa taarifa za kuahirishwa kwa kongamano hilo ili kupunguza idadi ya washiriki wake,” alisema.

Aidha, alisema baada ya kushindwa kwa vitimbi vyao hivyo, siku ambayo kongamano hilo lilipangwa kufanyika, Jeshi la Polisi liliamua kuvamia ukumbi wa kongamano, kuwalazimisha waandaaji kuvunja kongamano hilo na kuwazuia waalikwa kuingia ukumbini.

Alisema kutokana na waandaaji wa kongamano hilo kutaka kujua msingi wa uamuzi wa jeshi hilo kuvamia na kuzuia shughuli hiyo.

Hata hivyo, alisema licha ya jeshi hilo kuvunja kongamano hilo, hawatovunjika moyo na badala yake wamechochea ari na hamasa na karibuni watatoa taarifa yingine ya kufanyika kwa kongamano lingine.

Akijibu tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nasir Ali, alisema jeshi lake halikuvunja kongamano hilo bali limekataza kutolewa mada za uchochezi ambazo alisema zilikuwa zimeshaandaliwa kutolewa katika kongamano hilo.

Kamanda Hassan alisema baada ya polisi kukataza mada za uchochezi, ndipo vijana hao walipoamua kuahirisha kongamano hilo ambalo lilipangwa kufunguliwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Habari Kubwa